Ancelotti ana nia kutomchezesha Torres

Meneja wa Chelsea Carlo Ancelott, amesema haogopi kumuweka nje Fernando Torres kwa mchezo wa marudiano kuwania Ubingwa wa Ulaya, hatua ya robo fainali ngwe ya pili dhidi ya Manchester United.

Haki miliki ya picha Other
Image caption Torres akipeana mkono na Ancelotti

Torres, tangu aliposajiliwa na Chelsea kwa kitita cha paundi milioni 50 akitokea Liverpool mwezi wa Januari, bado hajafunga bao hata moja.

Na alipoulizwa iwapo anahofia iwapo mmiliki wa timu Roman Abramovich atachukia kwa kutomchezesha Torres, Ancelotti alisema: "Hapana. Kamwe sifikirii hilo.

"Roman ni mtu mwenye akili sana, hajawahi kunitaka nifanya jambo kama hilo."

Ancelotti ameshutumiwa kwa kuendelea kumchezesha Torres katika mchezo wa awali walipofungwa na bao 1-0 na Manchester United katika uwanja wa Stamford Bridge siku ya Jumatano, huku Didier Drogba akipumzishwa licha ya kucheza vizuri ikilinganishwa na Torres.

Na kumekuwa na uvumi kwamba kusajiliwa kwa Torres ambaye pia ni mshambuliaji wa timu ya taifa ya Hispania, ilikuwa ni matakwa ya Abramovich, kitu ambacho kila mara Ancelotti amekuwa akikanusha.

Na Ancelotti ameongeza: "Fernando bila shaka huenda asianze kucheza dhidi ya United.

"Kwa nini isiwezekane? Ninawajibika kuchagua kikosi imara zaidi. Kuna ushindani mkubwa katika safu ya ushambuliaji na chochote kinawezekana.

"Nitachagua wachezaji, na sio kufanya ulinganifu wa uwezo wa wachezaji kutokana pesa ambazo klabu inawalipa.

"Nitachagua wachezaji kutokana na wanavyojituma mazoezini, na hali pamoja na ari ya wachezaji. Fernando analifahamu hili fika."

Ancelotti, ambaye alimuuza Andriy Shevchenko kwa Chelsea wakati akiifundisha AC Milan, amekataa kulinganishwa na na suala hili.

Shevchenko ni mshambuliaji mwengine inaarifiwa alisajiliwa kutokana na mapenzi ya Abramovich, na akadhihirisha kuwa ni mchezaji ghali ambaye hakuweza kuwika.