Wenger asema nafasi ya pili si "maafa"

Arsene Wenger amesisitiza kushindwa kushinda kombe kwa misimu sita mfululizo haitakuwa "maafa" kwa Arsenal.

Image caption Arsene Wenger

Chama cha mashabiki wa Arsenal ambao pia wana hisa katika klabu hiyo, hivi karibuni walionesha masikitiko kutokana na matokeo yasiyoridhisha kwa timu hiyo.

Meneja huyo wa Gunners amesema: "Tupo nafasi ya pili ya msimamo wa ligi. Hiyo utaita maafa? Kuna baadhi ya timu ambazo zimewekeza mara 10 kushinda sisi, na bado zipo nyuma yetu.

"Baadhi ya vilabu vipo nyuma yetu na hivijafanya la maana kwa miaka 20, na bado wanapongezwa. Sielewi."

Ameongeza: "Iwapo tunavunjika moyo mwishoni mwa msimu, basi ni sawa. Kwa nini useme ni maafa wakati tunashikilia nafasi ya pili ya ligi? Je vilabu 18 vilivyo nyuma yetu vilikuwa na msimu mzuri sana?"

Arsenal wanashikilia nafasi ya pili ya masimamo wa ligi, nyuma ya Manchester United, lakini walitolewa katika mashindano ya kuwania Kombe la FA na Ligi ya mabingwa wa Ulaya wiki sita zilizopita na pia wakapoteza mchezo wa fainali ya Kombe la Carling dhidi ya Birmingham.

Hawajashinda kombe tangu mwaka 2005 waliponyakua kombe la FA - lakini wamedumu katika nafasi nne za mwanzo za msimamo wa ligi ya England, hali inayowawezesha kuwa washiriki wa kudumu wa mashindano ya ligi ya Mabingwa wa Ulaya kila msimu.

Na Wenger anataka lawama zozote kwa timu yake zielekezwe kwa kusingatia muktadha, akisisitiza wanaelekea katika njia sahihi.

Wenger ameendelea kueleza: "Tumekuwa katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kwa miaka 15, na kuna vilabu viwili tu vilivyofanya hivyo katika nchi hii na kubainisha ni wao na Manchester United.