Jeshi la Gbagbo Bado Limevinjari

Mkuu wa kikosi cha amani cha Umoja wa Mataifa, Alain Leroy, akizungumza kutoka makao makuu mjini New York, amesema majeshi ya Laurant Gbagbo yamesonga mbele, na yanadhibiti kabisa mitaa ya Cocody, kati-kati ya Abidjan.

Mwandishi wa BBC, Mark Doyle, yuko Cocody na anasema mapigano makali yanaendelea huko, ambayo yanaonesha, pengine hakuna upande unaodhibiti eneo hilo kikamilifu.

Mwandishi huyo wa BBC anasema mapigano yanaendelea karibu na hapo alipo, ambapo ni kama kilomita moja au mbili kutoka nyumba ya Laurent Ghabgbo, kiongozi wa sasa wa Ivory Coast, ambaye anakataa kuondoka madarakani.

Haki miliki ya picha Reuters

Anasema ni wazi kuwa mapambano yanaendelea, na wanajeshi wa Ufaransa wako kati ya mapigano hayo.

Na Shirika la Kupigania haki za Kibinaadamu, Human Rights Watch, limewashutumu wafuasi wa ma-rais wawili wa Ivory Coast wanaozozana, kwamba wamekiuka haki za kibinaadamu.

Linasema, wapiganaji wa Alassane Ouattara wameuwa mamia ya raia, na kuwanajisi wafuasi wengi wa Laurent Gbagbo.

Piya shirika hilo linasema, majeshi ya Bwana Ouattara yalichoma moto vijiji kama kumi katika eneo la magharibi.

Wakati huo-huo, Human Rights Watch inaeleza kuwa wanajeshi wa Laurent Gbagbo wamewauwa wapinzaani wao mia moja, kaskazini mwa Ivory Coast.

Shirika hilo limetoa wito kwa Bwana Ouattara kufanya uchunguzi unaoaminika na ulio huru, juu ya tuhuma hizo.