Arsenal yacharuka yailaza Blackpool 3-1

Arsenal wamefufua matumaini yao haba ya kutwaa ubingwa baada ya kuilaza Blackpool mabao 3-1 nyumbani kwao na kuwaacha wenyeji wakiwa pointi moja tu ya mstari wa kushuka daraja.

Mlinda mlango mkongwe Jens Lehmann, mwenye umri wa miaka 41, alianza kucheza mechi hiyo baada ya Manuel Almunia kuumia dakika chache kabla ya mpira kuanza.

Lakini Arsenal ilicharuka dakika za mwanzo na kupata mabao mawili ya haraka haraka katika dakika ya 21 akianza Abou Diaby na dakika tatu baadae Emmanuel Eboue akaandika bao la pili.

Gary Taylor-Fletcher aliifungia Blackpool bao moja kipindi cha pili baada ya wenyeji kucharuka na kuliandama lango la Arsenal na ikaonekana kama wangewaweka Arsenal katika wakati mgumu, lakini Robin Van Persie alidhoofisha matumaini ya Blackpool kwa kufunga bao la tatu zikiwa zimesalia dakika 15 kabla mpira kumalizika baada ya pasi nzuri ya Theo Walcott.

Blackpool walikosa nafasi nzuri ya kufunga bao baada ya Lehmann kuokoa mkwaju wa chini chini wa Campbell - lakini Arsenal sasa watarejea London wakiwa na matumaini makubwa ya kukamilisha ndoto yao ya kushinda ubingwa wa ligi.

Arsenal wamefikisha pointi 62 wakiwa nafasi ya pili ya msimamo wa ligi, huku wamecheza mechi 31 dhidi ya 32 walizocheza vinara wa ligi hiyo kwa sasa Manchester United, wenye pointi 69.