Japan inatoa ratiba ya kinu cha nuklia

Kampuni ya umeme ya Japan, Tepco, inayomiliki kinu cha nuklia cha umeme kilichoharibika, inasema inaweza kuchukua hadi mwisho wa mwaka kutengeneza kinu hicho.

Tepco, ilisema inakusudia kupunguza taratibu, kiwango cha mionzi inayovuja kutoka kinu kilioko Fukushima, katika miezi mitatu ijayo, na kukipoza kinu hadi kuweza kukifunga katika miezi sita hadi tisa.

Haki miliki ya picha AFP

Tangazo hilo limetolewa wakati wa ziara ya Waziri wa Mashauri ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton.

Bi Clinton ameahidi kuwa Marekani itaisaidia Japan wakati inashughulika na uharibifu uliosababishwa na tetemeko la ardhi na tsunami ya mwezi uliopita.

Meli na ndege kadha za Marekani, pamoja na wanajeshi 20,000, walishiriki katika uokozi baada ya maafa.

Katika siku chache za karibuni, kiwango cha mionzi ya nuklia kimezidi katika pwani karibu na Fukushima, na kampuni ya nishati ya TEPCO imechagizwa na serikali kueleza mpango wa kumaliza uchafuzi huo

Mwenyekiti wa Tepco, Tsunehisa Katsumata, amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari, kwamba jambo muhimu ni kuepusha mripuko mwengine wa hydrogen usitokee katika kinu hicho, na kuzuwia maji yenye mionzi kuvuja na kudondoka kwenye bahari ya Pacific.