Imarati itapatanisha Yemen

Maduka na biashara nyingi zimefungwa leo nchini Yemen, wakati watu wanashiriki katika maandamano ya amani dhidi ya Rais Ali Abdullah Saleh.

Na maandamano mengine dhidi ya serikali yanafanywa katika miji kadha.

Waziri wa Mashauri ya Nchi za Nje wa Imarati anatarajiwa nchini Yemen hii leo, kujadili pendekezo la nchi za Ghuba, kwamba Rais Saleh akabidhi madaraka kwa makamo wake katika muda wa mwezi mmoja.

Hapo jana Bwana Saleh alisema anakaribisha mpango huo, na atalishughulikia pendekezo kufwatana na katiba ya Yemen.

Mpango wa nchi za Ghuba unapendekeza kuwa Bwana Saleh ahakikishiwe kuwa yeye, familia yake na wasaidizi wake, hawatashtakiwa - jambo ambalo limekataliwa na upinzani.

Zaidi ya watu 100 wamekufa katika miezi miwili ya maandamano, kutaka Rais Saleh ang'atuke.