Vyuo Vikuu Afrika havitambuliwi

Haki miliki ya picha other
Image caption Chuo kikuu cha Khartoum

Kuorodhesha vyuo vikuu kulingana na umaarufu ni desturi inayokua kwa kasi sana katika sekta ya elimu ya juu.

Orodha hiyo, inayojumuisha vyuo vikuu vilivyo maarufu zaidi duniani, ina walakini kwani bara zima halimo.

Hutapata hata chuo kimoja kutoka bara la Afrika kwenye orodha hiyo.

Vyuo vikuu vilivyoorodheshwa ni vya Marekani, Ulaya na baadhi kutoka China na Korea Kusini huku Afrika ikiwa imesahaulika.

Mazungumzo yanayohusu utandawazi wa vyuo vikuu yanatumia lugha ya kuvutia iliyorembwa kwa mada ya ushirikiano wa kimataifa, pamoja na mzunguko wa fedha katika mitandao ya kimataifa.

Ni rahisi sana kupotoshwa na mafanikio ya vyuo hivi ambavyo mazoea ni kuwatunukia watu tuzo na kujionyesha.

Swali ni, ikiwa ushindani wa kimataifa wa vyuo hivi utajikita katika hadhi na uwezo wa vyuo vichache, na hivyo basi bara zima likasahaulika, mambo yatakuwa vipi?

Idadi yaongezeka

Kwa mujibu wa taasisi ya takwimu ya shirika la elimu, sayansi, na utamaduni la Umoja wa Mataifa, kuna wanafunzi milioni 4.5 kusini mwa jangwa la Sahara.

Kulingana na orodha hiyo, wanafunzi hawa kutoka bara la Afrika ni kama hawapo.

Haki miliki ya picha other
Image caption Bw Thandika Mkandawire

Lakini idadi hii inawakilisha kuwepo kwa ongezeko kubwa. Mwaka 1970, idadi ya wanafunzi Ilikuwa 200,000 katika eneo hilo la Afrika na sasa idadi ya vijana wanaojiunga na chuo kikuu imeongezeka kutoka aslimia moja hadi sita.

Katika takwimu hizi kuna tofauti kubwa zinazojitokeza. Nchini Malawi, takriban asilimia 0.5 ya vijana watajiunga na chuo kikuu wakati Cameroon kiwango kimefikia asilimia tisa.

Pia kuna mienendo tofauti kwa wale wanaoamua kusomea ng'ambo.

Wanafunzi wanaotoka kusini mwa jangwa la Sahara wengi wao husomea nchi za Afrika Kusini na Ufaransa.

Pia wanafunzi kutoka Afrika Kaskazini huenda kusomea Ufaransa.

Tatizo lingine ni kwamba wanawake kutoka bara la Afrika huwa hawajiungi na chuo kikuu kwa wingi.

Ukilinganisha idadi ya wanawake na wanaume katika vyuo vikuu, idadi ya wanaume ndio kubwa zaidi.

Nchini Chad - nchi iliyo kubwa zaidi kushinda nchi za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zikijumuishwa pamoja - asilimia 0.6 pekee ya wanawake ndio wanaojiunga na chuo kikuu.

Ingawa idadi ya wanafunzi kuongezeka barani Afrika ni jambo zuri, hii itaathiri mambo mengine pia.

Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Dunia, ongezeko la idadi ya wanaojiunga na chuo kikuu imeongezeka mno hata kuzidi uwezo wa kifedha wa vyuo hivyo kuajiri wafanyakazi na kununua vifaa.

Mwelekeo tofauti wa ufadhili

Profesa Thandika Mkandawire, mkufunzi wa maendeleo barani Afrika 'African Development' katika chuo kikuu cha LSE alisema, vyuo vikuu vya Afrika bado vinajaribu kurudi katika hali yake kutokana na kukosa ufadhili miaka ya 80 baada ya fedha hizo kuhamishwa kwenye shule za msingi.

Katika enzi za baada ya ukoloni kwenye miaka ya 60 na 70, vyuo vikuu vingi viliibuka barani Afrika lakini hali hii ilisitishwa ghafla. Na wakati maeneo mengine duniani yalikuwa yakiwekeza kwenye elimu ya juu, bara la Afrika lilikosa fursa hiyo.

Profesa Mkandawire alisema "Ukishaangamiza chuo kikuu, ustawishaji wa chuo hicho tena utakuwa si rahisi."

Haki miliki ya picha other
Image caption Waandamanaji wadai uwekezaji kwenye elimu

Huenda itakuwa vigumu sana kujaribu kukaribia vipimo vya maendeleo vilivyoko katika vyuo vikuu vingine duniani baada ya 'miaka mingi' iliyopotezwa.

Prof Mkandawire alisema, watu wenye kipato cha kawaida wanajitahidi kushinikiza kuwepo kwa vyuo bora zaidi ili ijadiliwe kwenye duru za kisiasa.

Pia kuna ufahamu kuwa vyuo vikuu ni sekta mojawapo iliyo muhimu katika kuujenga uchumi wa kisasa.

Jo Beall, makamu mkuu wa chuo kikuu cha Cape Town Afrika Kusini (chuo pekee kutoka Afrika kuwa miongoni mwa vyuo vikuu 200 vilivyo bora) alisema "Vyuo vikuu ndio pahala panapo fursa ya kujipandisha katika tabaka za kijamii."

Rasilmali yaadimika

Bi Beall alielezea jinsi alivyoona barabara za kuelekea chuo kikuu kimoja Afrika ya kati zikiwa zimejaa foleni za watu wakiwa na mashine ya kupiga chapa ili kutoa huduma kwa wanafunzi, zikiwa zinaendesha na betri za gari, wakiwa wananakili vitabu vya miaka ya 50.

Wanafunzi hulazimika kusafiri kwa saa tatu au nne ili kufika chuo kikuu.

Haki miliki ya picha other
Image caption Wasiwasi wa kisiasa umekuwa kikwazo kwa uwekezaji barani Afrika.

Isitoshe, ukumbi wa mihadhara hujaa kupindukia hadi kuna walinzi na lango la kudhibiti msongamano wa watu.

Profesa Beall ambaye atajiunga na taasisi ya 'British Council' baadaye mwaka huu alisema, licha ya hayo, bado ana matumaini kuhusu mustakabali wa mfumo wa elimu ya juu Afrika.

Kuna vyuo vikuu vinavyojitahidi kuwa taasisi zinazojishughulisha na utafiti wa hali ya juu.

Phillp Altbach, mkurugenzi wa 'Centre for International Higher Education Boston College' Marekani alisema udhaifu wa vyuo vikuu barani Afrika haitokani tu na ukosefu wa fedha bali kuna kasoro kadha wa kadha ikiwa ni pamoja na msukosuko wa kisiasa na ubadhirifu wa mali.

Kushindwa kuvutia

Soko la wanafunzi kutoka nje halijafanikiwa kuwavutia wanafunzi kwenda barani Afrika. Badala yake, wasomi wamelihama bara hilo kwenda kuishi ng'ambo.

Haki miliki ya picha other
Image caption Chuo kikuu Tunis

Vyuo vikuu vya Marekani na Uingereza vimewekeza katika matawi ya vyuo vyao barani Asia na Mashariki ya kati badala ya Afrika.

Pia Afrika, ambapo utajiri mkubwa sana na umaskini uliokithiri, umekosa watu wenye uwezo wa wastani Afrika hawana ushawishi kama wale wanaoishi nchi za China na India ambako wamechochea ustawishaji wa elimu ya juu nchini mwao.

Pamoja na uwekezaji wa fedha, alisema kunahitajika mabadiliko ya kitamaduni kama vile kulinda uhuru wa kitaaluma ili kuweka hali itakayoimarisha vyuo vikuu.

Lakini hakuna kuepuka pengo la kiuchumi.

Aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair ameunda wakfu inayofanya kazi na mtandao wa vyuo vikuu duniani kote, ikiwemo Afrika na Marekani.

Alisema chuo kikuu cha Yale, Marekani si tu kwamba kina uwezo mkubwa kifedha na chuo kama cha Fourah Bay College Sierra Leone - mali iliyowekwa wakfu ya Yale ni mara chungu nzima zaidi ya utajiri wa nchi nzima.

Ruth Turner mkurugezi mkuu wa wakfu hiyo alisema tofauti hii illiopo kwa sasa haitokani na hali ya uchumi tu bali kunahitajika kuliangalia suala hili kwa misingi ya maadili.

"Sote tunaishi katika dunia ya utandawazi lakini tunakosa namna ya kujadili tatizo hili tukizingatia maadili."

Maendeleo ya kiuchumi

Katika utandawazi duniani, vyuo vikuu vyenye uwezo vinaonekana kunufaika zaidi na vile vilivyo maarufu zaidi.

Haki miliki ya picha other
Image caption Chuo kikuu cha Free State

Vyuo vikuu vilivyo katika mstari wa mbele ni "taasisi za kimataifa. Vyuo hivi vinaweza kuwavutia wakufunzi waliobobea na vina uhusiano na sekta ya biashara pamoja na kuwa na ushawishi uliovuka mipaka" alisema Keith Harman ambaye anafanya kazi kwenye mradi unaofadhiliwa na jumuiya ya madola kuendeleza vyuo vikuu nchini Uganda ili kuwavutia wanafunzi wa Afrika mashariki na kusini.

Kwa upande mwingine, vyuo vikuu vingi barani Afrika ambavyo havina uhusiano kama huo "manufaa ya utandawazi "

"Vyuo vikuu ni misingi muhimu ya kuwaleta watu waliostadi na pia vina umuhimu katika kuleta maendeleo ya kiuchumi" alisema Bw Harman lakini vyuo vingi Afrika vinapoteza fursa ya kupanda daraja kwani havijafanikiwa katka uwekezaji na utafiti zaidi, pamoja na uwezo wa kuwavutia wanafunzi kutoka ng'ambo.

Profesa Makandawire alisema hata hivyo, kuna dalili za kuwepo na matumaini. " Kuna mabadiliko, mambo yanakuwa wazi zaidi ; ukandamizaji umepungua."

Alisema pia kuna ufahamu kuwa kusitisha uwekezaji katika vyuo vikuu ilikuwa ni makosa ambayo sasa yanarekebishwa.

Aliongezea "Kuna matokeo mazuri ambayo yanayojitokeza" lakini alitoa ilani kuwa maendeleo yatachukua miaka mingi ya kazi ngumu.