CCM Tanzania yafanya 'usafi'

Hatimaye chama kinachotawala nchini Tanzania - Chama cha Mapinduzi - kimepata Katibu Mkuu mpya ambapo pia kimewatoa viongozi wake wote wanaotuhumiwa kwa ufisadi.

Image caption Wilson Mukama

Katibu Mkuu huyo mpya ni Wilson Mkama ambaye anachukuwa nafasi iliyoachwa wazi na Katibu Mkuu aliyemtangulia Yusuf Makamba.

Aidha Chama hicho kimetangaza sekretarieti mpya na majina ya watakaounda Kamati Kuu ya chama hicho kuziba nafasi zilizoachwa wazi na wajumbe waliojiuzulu usiku wa kuamkia Jumapili.

Walioteuliwa kuunda sekretarieti ya chama hicho ni Wilsom Mukama Katibu Mkuu, John Chiligati Naibu Katibu Mkuu (Bara) na Vuai Ali Vuai Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar).

Wengine ni Nape Nnauye ambaye anakuwa Katibu wa Itakadi na Uenezi, Januari Makamba Katibu Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa na Mwigulu Nchemba ambaye anakuwa Katibu wa Uchumi na Fedha.

Katika hatua nyingine chama hicho kimetangaza vita dhidi ya wanachama wa chama hicho wanaotuhumiwa na kashfa za ufisadi na kuwataka wajiondoe wenyewe kwenye nafasi walizonazo ndani ya chama.

Naibu Katibu Mkuu John Chiligati amesema kama wanachama hao wasipojiwajibisha wenyewe chama hicho hakitasita kuwatimua mara moja.

“Wale wote wanaotajwatajwa katika kashfa mbali mbali kama ya Richmond, Kagoda, Dowans hata kama hatuna ushahidi lakini kwa vile jamii inawatuhumu tumewataka wajipime wachukue hatua za kujiuzulu kuwa wajumbe Halmashauri Kuu. La wasipotekeleza maazimio hayo Chama kitawawajibisha.” Amesema Chiligati.