Hunta kushiriki mbio za wanawake

Shirikisho la kimataifa la riadha duniani IAAF limepitisha kanuni mpya kwamba hunta wataruhusiwa kushiriki katika mbio za wanawake.

Image caption Caster Semenya

Hatua hiyo imefuatia baraza la IAAF kupitia sheria zake kufuatia utata uliozuka katika sakata la mwanariadha wa Afrika Kusini Caster Semenya.

Semenya alishinda mbio za ubingwa wa dunia mita 800 mwaka 2009 mjini Berlin, lakini IAAF ilisitisha kumtambua hadi uchunguzi ufanyike.

Kanuni hizo zitaanza kufanya kazi Mei Mosi mwaka huu.

Watu wenye hali ya hunta huwa na viwango vikubwa vya androgen, na wanariadha wa kike wenye hali hiyo, chini ya sheria za zamani, walizuiwa kushiriki katika michuano, kama ilivyokuwa kwa Semenya.

Semenya tayari amerejea kushiriki katika michunao, lakini sakata hilo lilisababisha baraza la IAAF kupitia upya kanuni zake jambo lililochukua miezi 18.

Vipimo vya wanawake hutofautiana na wanaume, kwa sababu wanaume huwa na androgen nyingi zaidi. Mwanariadha wa kike ataruhusiwa kushiriki katika mbio za wanawake iwapo viwango vya androgen viko chini ya viwango vya kawaida vya wanaume.