Fukushima bado inafukuta

Maafisa nchini Japan wamesema hali ya dharura katika kinu cha nuklia cha Fukushima kiwango cha kutoka kwa chembechembe za mionzi kimefika saba, kwa vipimo vya kimataifa vya ajali zinazotokea za mitambo ya nuklia.

Haki miliki ya picha Other
Image caption Mtambo wa Fukushima

Kiwango hicho kinaonyesha jumla ya athari ya mionzi inayotokana na kuvuja kwa nyuklia kutoka kwenye kinu kilichoharibiwa cha Fukushima Daiichi ikilinganishwa na hapo awali.

Kiwango cha saba kilitumika mara ya mwisho mwaka 1986 wakati wa janga la Chernobyl na kiwango cha mionzi kilikuwa mara kumi zaidi. Waziri mkuu wa Japan Naito Kan amesema kiwango cha mionzi inayovuja kutoka katika kinu hicho kinapungua.

Shirika la umeme la Tokyo linaloendesha mtambo huo punde litatoa utaratibu wa kuudhibiti.

“Hatua kwa hatua mitambo ndani ya kinu hicho cha Fukushima inaelekea kutengemaa” alisema.

Hakujawa na taarifa zozote za majeruhi wanaotokana na athari za kuvuja kwa kinu hicho, kadhalika hali ya hatari kwa binadamu kiafya inafikiriwa kupungua.

Wakati huo huo tetemeko lililotokea Jumanne lenye ukubwa wa kipimo cha 6.0 lilisababisha wafanyakazi wa kinu hicho kuondoka katika eneo la kazi.

Shirika la umeme Japan linasema linaangalia hali ya kiwanda baada ya tetemeko hili la pili kutokea siku kadhaa baada ya lile la kwanza lakini limesema hakujawa na taarifa za matatizo kutoka mtambo wa nje.

Athari zake zimekuja baada ya tetemeko kubwa na Tsunami kulikumba eneo la Kaskazini mashariki mwa Japan na kusababisha vifo vya watu 13, 228 na wengine 14, 529 hawajulikani waliko . Zaidi ya watu 15, 000 wamekosa makazi.