Misri:Mubarak kuhojiwa juu ya mauaji

Hosni Mubarak Haki miliki ya picha BBC World Service

Aliyekuwa rais wa Misri Hosni Mubarak ametakiwa kufika mbele ya mwendesha mashtaka mwandamizi wa serikali kuhojiwa juu ya madai ya ufisadi na mauaji ya waandamanaji.

Tangazo hilo limejiri muda mfupi baada ya Bwana Mubarak kutoa taarifa yake ya kwanza tangu kuondolewa madarakani miezi miwili iliopita,akikanusha madai ya ufisadi.

Kiongozi huyo wa zamani amesema ana haki ya kutetea heshima yake na akakanusha kuwa na mali yoyote katika nchi za kigeni.

Watoto wa Mubarak Gamal na Alaa pia wametakiwa kufika kwa mahojiano.

Mwendesha mashtaka mwandamizi amesema taarifa ya Mubarak, haitoathiri kwa vyovyote uchunguzi huo.

Siku ya Ijumaa,eneo la Tahrir mjini Cairo lilikuwa na waandamanaji wakitaka Bwana Mubarak na jamii yake kushtakiwa kwa ufisadi.

Mtu mmoja aliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa wakati maafisa wa usalama walipoingia kufukuza walioandamana.Walikuwa na majeraha ya risasi lakini jeshi lilikanusha kutumia risasi za moto.

Waandamanaji na wanaharakati wanaopinga ufisadi wamekuwa wakishinikiza kufanyiwa uchunguzi mali za familia ya Mubarak,zinazosemekana kuwa kati ya $1bn hadi $70bn.