Serikali ya Somalia kususia kongamano la UN

Mohamed Abdillahi, waziri mkuu wa somalia Haki miliki ya picha other

Kongamano la Umoja wa Mataifa kujadili hali ya Somalia pamoja na hatima ya serikali ya mpito ambayo kipindi chake kinamalizika mwezi Agosti mwaka huu linaanza juma hili mjini Nairobi.

Kikao hicho kinaanza huku Waziri Mkuu wa Somalia Mohammed Abdullahi akitangaza kususia na kusisitiza kwamba masuala yote ikiwemo mashirika ya kusaidia Somalia yanafaa kuwa mjini Mogadishu.

Zaidi ya wafanyakazi elfu moja wanaotoa misaada kwa Somalia wanaendesha shughuli zao kutoka Kenya

Serikali ya mpito ya Somalia imesema itasusia mkutano ulioandaliwa na umoja wa mataifa mjini Nairobi juma hili.Waziri mkuu wa Somalia Mohammed Abdullahi anasema wanasusia mkutano huo kwa kuwa walitaka mkutano ufanyike mjini Mogadishu.

Mkutano huu umependekezwa na mjumbe maalum wa umoja wa mataifa juu ya mzozo wa Somalia Augustine Mahiga,na ulikuwa na nia wa kuleta pande zote zinazozozana nchini humo pamoja.

Serikali ya Somalia inataka mashirika yote ya umoja wa mataifa ihamishie shughuli zake nchini Somalia

''Sisi tunajua mashirika ya umoja wa mataifa yametumia pesa nyingi mamilioni ya madola hata pengine dola bilioni moja na tunataka wawe karibu na watu wanaodai wanawahudumia na pia tunataka wajionee hali ilivyo wenyewe Somalia'' alisema waziri mkuu.

Tayari baadhi ya wajumbe wameanza kuwasili mjini Nairobi tayari kwa mkutano.Mkutano huo wa siku mbili unatarajiwa kuanza siku ya Jumanne.