Bougherra na Diouf waepuka adhabu zaidi

Madjid Bougherra na El-Hadji Diouf kwa pamoja wamepigwa faini, lakini wameepuka adhabu zaidi ya kufungiwa kutokana na utovu wa nidhamu walioonesha wakati timu yao ya Rangers ilipofungwa na Celtic katika kuwania Kombe la Scotland.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption El Hadji Diouf

Wachezaji hao wawili walitolewa nje baada ya kuoneshwa kadi nyekundu na walikuwa wakikabilia na mashtaka mengine ya "utovu wa nidhamu uliofurutu ada".

Diouf alipigwa faini ya paundi 5,000 na Chama cha Kandanda cha Scotland- SFA, wakati Bougherra yeye ametozwa faini ya paundi 2,500.

Meneja msaidizi wa Rangers Ally McCoist anasubiri uamuzi utakaotolewa wa rufaa yake akipinga kufungiwa mechi mbili kuwepo eneo la ufundi la timu hiyo uwanjani.

Rangers inapinga adhabu ya moja kwa moja aliyopewa McCoist, ambayo ilitolewa baada ya kutunishiana kifua baada ya mchezo kumalizika na meneja wa Celtic Neil Lennon.

Lennon tayari ameshapewa adhabu ya kufungiwa mechi nne kukaa eneo la ufundi la timu hiyo na mashtaka yake pia yameibua adhabu ya kusimamishwa mechi nyingine nne.

Hata hivyo SFA baadae iliafiki adhabu hizo za Lennon atazitumikia kwa wakati mmoja, kufuatia klabu ya Celtic kupinga adhabu hizo kisheria na meneja huyo atakuwepo katika benchi la ufundi la Celtic siku ya Jumanne usiku katika mechi dhdi ya St Johnstone.

Mapema katika kikao chake Chama cha Soka cha Scotland - SFA- kilisikiliza shauri la wachezaji hao wawili siku ya Jumanne na Diouf pamoja na Bougherra wameonywa kuhusiana na tabia zao siku zijazo.

Bougherra mchezaji wa timu ya taifa ya Algeria, kwa sasa hachezi soka kutokana na kuumia misuli, alikuwa mchezaji mmoja kati ya wawili wa Rangers waliotolewa wakati wa mechi dhidi ya Celtic Park tarehe 2 mwezi wa Machi - mwengine akiwa Steven Whittaker, wakati Diouf anayechezea timu hiyo kwa mkopo akitokea Blackburn alioneshwa kadi nyekundu baada ya filimbi ya mwisho.