Kufungwa Man City, Mancini abeba lawama

Meneja wa Manchester City Roberto Mancini amebeba lawama kutokana na timu yake kuchakazwa mabao 3-0 na Liverpool katika mchezo wa Ligi Kuu ya England.

Image caption Roberto Mancini

Mabao mawili ya Andy Carroll yaliidhoofisha Manchester City wakidemadema kupata nafasi nne za juu za kucheza Ligi ya Ubingwa wa Ulaya, wakishikilia nafasi ya nne, pointi tatu mbele ya Tottenham ambao wana mchezo mmoja mkononi.

"Hatukucheza vizuri dakika 20 za mwanzo wakati Liverpool walicheza vizuri, lakini usiku huu nilifanya makosa. Ni makosa yangu. Tungeweza kufanya vizuri," Alisema Mancini.

Alifanya mabadiliko ya wachezaji watatu waliocheza katika mechi waliyoifunga Sunderland mabao 5-0 wiki iliyopita.

Bado Manchester City wanakibarua kujiandaa kwa ajili ya mchezo wa siku ya Jumamosi wa nusu fainali Kombe la FA dhidi ya mahasimu wao wakuu Manchester United katika uwanja wa Wembley.

Zaidi ya kuwa na usiku mbaya, Manchester City imepata pigo jingine baada ya mshambuliaji wao wa kutumainiwa Carlos Tevez kuumia misuli ya paja, ikiwa na maana huenda mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Argentine huenda asicheze mechi dhidi ya Manchester United.

Bila ya kuzama kwa kina juu ya makosa anayosema ameyafanya, Mancini ameongeza: "Ninawaomba radhi mashabiki. Hata mimi mwenyewe nimefedheheshwa. Nimefanya makosa kwa mchezo huu na sio kwa wachezaji, wachezaji walicheza kwa kiwango chao cha asilimia 100.

"Nilifanya makosa katika siku mbili zilizopita, naelewa kwa nini. Ni muhimu kuelewa hili kwa ajili ya pambano lijalo. Ni makosa yangu kwa sababu hatukujiandaa vizuri."

Mshambuliaji Edin Dzeko, ambaye hajafunga katika mchezo wa ligi tangu alipojiunga na Manchester City akitokea Wolfsburg mwezi wa Januari, alichukua nafasi ya Mario Balotelli, ambaye awali aliingia badala ya Tevez, na kiungo Gareth Barry pamoja na James Milner waliingia badala ya Nigel de Jong na David Silva.

"Nilifanya mabadiliko ya wachezaji watatu, nikaingiza wachezaji watatu wapya, mtazamo wetu haukuwa sahihi," aliongeza Mancini. "Liverpool walicheza vizuri sana katika dakika 20 za mwanzo, tuliwaachia wacheze wanavyotaka, na walikuwa wakali mwanzoni na sisi tukawa tumepoa.