Szczesny na Djourou kucheza na Liverpool

Wachezaji wawili wa Arsenal Wojciech Szczesny na Johan Djourou wanajiandaa kurudi uwanjani siku ya Jumapili katika mchezo dhidi ya Liverpool.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Johan Djourou

Mlinda mlango Szczesny amepona baada ya kidole chake kuchomoka tarehe 8 mwezi wa Machi, Arsenal ilipocheza na Barcelona.

Djourou bega lake lilichomoka katika mechi dhidi ya Manchester United tarehe 12 mwezi wa Machi, lakini kama ilivyo kwa Szczesny amekwishaanza mazoezi kamili.

Mlinzi wa kati Thomas Vermaelen bado anaendelea vizuri baada ya kufanyiwa upasuaji wa kifundo cha mguu na Arsenal wanampangia kucheza mechi za kirafiki zisizokuwa na watazamaji.

Haijafahamika iwapo mlinzi huyo wa timu ya taifa ya Ubelgiji ataweza kucheza kikosi cha kwanza mwishoni mwa msimu, lakini inaaminika anaendelea vizuri sana.

Amekwishaanza mazoezi na hajisikii maumivu akikimbia na kupiga mpira, ingawa bado hajaanza mazoezi na kikosi cha kwanza.

Vermaelen hajacheza tangu alipoumia wakati akiichezea timu yake ya taifa katika mchezo wa kufuzu mashindano ya Euro 2012 dhidi ya Uturuki tarehe 7 mwezi wa Septemba.

Alifanyiwa upasuaji mwezi wa Januari na meneja wa Arsenal Arsene Wenger, alisema mwezi wa Machi hataweza kucheza kwa msimu huu wote.

Lakini Vermaelen aliliambia gazeti moja la Ubelgiji la Het Laatste Nieuws ana nafasi "finyu" kuweza kurejea kucheza kwa msimu huu.

Wakati huohuo, Szczesny na Djourou wanajiandaa kurejea kuitetea Arsenal katika mpambano muhimu dhidi ya Liverpool siku ya Jumapili.

Szczesny amekosa michezo minne tangu alipoumia kidole cha kati cha mkono wa kushoto, lakini baada ya kufanyiwa vipimo wiki iliyopita alionekana amepona na anaweza kudaka.

Baada ya ushindi wa siku ya Jumapili wa mabao 3-1 dhidi ya Blackpool, Wenger alisema, mlinda mlango huyo karibu atapona na atapangwa moja kwa moja kwa mchezo unaofuata.

Iwapo ataweza kucheza basi Jens Lehmann mwenye umri wa miaka 41 ataondolewa kama mlinda mlango wa akiba - labda tu Manuel Almunia, ambaye ni mlinda mlango namba mbili aonekane hajapona vizuri baada ya kuumia goti wakati wa kupasha moto viungo kabla ya mchezo dhidi ya Blackpool.

Djourou awali ilitazamiwa asingeweza kucheza hadi msimu huu utakapomalizika, lakini bega lake linaonekana halikuumia sana kama ilivyodhaniwa awali na anaweza kucheza baada ya kukosa mechi tatu.

Arsenal wapo pointi saba nyuma ya vinara wa Ligi Kuu ya England Manchester United wakiwa na mchezo mmoja mkononi, huku Manchester United Jumamosi hii wakiingia uwanjani dhidi ya Manchester City katika mchezo wa kuwania Kombe la FA, na kikosi cha Wenger kinaweza kupunguza wigo wa pointi hadi nne iwapo wataifunga Liverpool.