Onyo latolewa kwa ulipizaji kisasi

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Bw Alassane Ouatara na baadhi ya viongozi wenziwe

Shirika la kimataifa la Amnesty limesema Rais mpya wa Ivory Coast Alassane Ouattara lazima asimamishe mashambulio ya ulipizaji kisasi dhidi ya wafuasi wa mpinzani wake.

Shirika hilo lenye makao yake makuu nchini Uingereza limesema watu wenye silaha waliovaa sare walikuwa wakifanya msako wa kuwatafuta wafuasi wa Laurent Gbagbo nyumba baada ya nyumba mjini Abidjan.

Limesema, watu wengi upande wa magharibi wa nchi hiyo nao walishakimbia kujificha kwenye vichaka baada ya vijiji kuteketezwa.

Wafuasi wa Bw Ouattara walimkamata Bw Gbagbo siku ya Jumatatu baada ya kukataa kuachia madaraka.

Alikuwa akisistiza kuwa ameshinda uchaguzi wa urais wa mwezi Novemba, ijapokuwa majeshi ya kutunza amani ya Umoja wa Mataifa nchini humo ambayo yalikuwa yakisimamia uchaguzi huo yalisema Bw Ouattara alishinda.

Katika kipindi cha miezi minne ya mapigano baina ya Bw Gbagbo na Bw Ouattara takriban watu 1,500 waliuawa na milioni moja walilazimika kukimbia makazi yao.