Alex Ferguson asema Torres atawika tu

Sir Alex Ferguson amemtetea Fernando Torres, atakuwa mwiba kwa kupachika mabao upande wa Chelsea licha ya timu hiyo kufungwa 2-1 na Manchester United katika robo fainali ya marudio ya Ligi ya Ubingwa wa vilabu vya Ulaya.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Fernando Torres

Torres ambaye alisajiliwa kwa kitita cha paundi milioni 50, hajafunga bao tangu alipochukuliwa na Chelsea mwezi wa Januari na alibadilishwa kipindi cha pili, wakati Chelsea walipotolewa katika mashindano hayo kwa jumla ya mabao 3-1.

"Sioni kwa nini waamue kumuache baada ya kumsajili kwa kitita kikubwa cha pesa," alisema meneja wa Manchester United Ferguson.

"Kwa wakati huu hajaweza kuonesha cheche zake, lakini bado ni kijana na kuna misimu zaidi inakuja."

Mengi yamesemwa kutokana na uamuzi wa meneja wa Chelsea Carlo Ancelotti kumuanzisha Torres badala ya Didier Drogba.

Ancelotti alipoulizwa iwapo alikosea kumchezesha Torres badala ya Drogba, alijibu: "Pengine. Inawezekana. Nimekwishawaeleza mara nyingi msimu huu, ninapendelea kumuanzisha Fernando kwa aina ya mchezo kama huu na mbinu kama hizi.

Aliongeza: "Didier alicheza vizuri kipindi cha pili. Nilitaka kuongeza mashambilio zaidi kwa sababu tulitaka kushinda. Didier alikuwa bado damu inamchemka na angeweza kutumia nguvu zake mstari wa mbele. Hii ndio sababu iliyonifanya nimtoe Fernando."

Wakati huo huo, Ancelotti amekiri Manchester United walistahili kushinda mchezo dhidi yao uliyochezwa uwanja wa Old Trafford usiki wa Jumanne.

"Tulimiliki mpira kwa dakika 25 za awali lakini tukashindwa kufunga," aliongeza.

"Mwishoni mwa kipindi cha kwanza walipofunga, hali ilikuwa ngumu kwa upande wetu, tulicheza tukiwa 10, lakini mwisho wa mchezo tulishindwa.

Chelsea imekwishatolewa katika mashindano yote ya kuwania vikombe na kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu ya msimamo wa Ligi Kuu ya England, wakiwa pointi 11 nyuma ya vinara wa ligi hiyo Manchester United.

Alipoulizwa kuhusu jukumu la kuinua ari ya wachezaji wake, Ancelotti aliongeza: "Itakuwa vigumu lakini hatuna budi kufanya kila liwezekanalo kushika nafasi nne za juu za Ligi ili tucheze Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu ujao.