Besigye wa Uganda apigwa risasi mkono

Dk Kizza Besigye Haki miliki ya picha Majimbo Kenya
Image caption Besigye amekuwa akitembea kwenda kazini kama njia moja ya kufanya maandamano

Habari kutoka nchini Uganda zinasema kwamba kiongozi wa upinzani nchini humo Kizza Besigye amepigwa risasi ya mkono na maafisa wa polisi ambao walikuwa wakijaribu kuwatawanya watu waliokuwa wakiandamana na kiongozi huyo wa upinzani mjini Kampala.

Awali polisi walijaribu kumzuia Besigye kutembea kwa miguu hadi kazini kama sehemu ya maandamano ya kupinga ongezeko la gharama ya maisha, lakini juhudi zao ziligonga mwamba baada ya raia kumzingira Besigye.

Watu kadhaa wakiwemo wabunge wawili wamekamatwa na polisi.

Kumekuwa na taarifa pia za maafisa wa polisi kutumia gesi ya kutoa machozi katika hospitali moja, baada ya waandamanaji kuanza kuwapura kwa mawe, walipokuwa wakiandamana na kulalamika juu ya ongezeko kubwa la bei za bidhaa muhimu na mafuta.

Mfanyakazi mmoja wa hospitali hiyo katika mji wa Kasangati, nje kidogo ya mji mkuu wa Kampala, amesema baadhi ya kina mama waliokuwa na watoto wagonjwa katika hospitali hiyo iliwabidi kuwahamisha watoto ili wasiathiriwe kwa gesi hiyo ya kutoa machozi.

Besigye kwanza alikamatwa siku ya Jumatatu, akiwa pamoja na wabunge wachache, waliokuwa wakishiriki katika maandamano kama ya leo.

Siku ya Alhamisi alikamatwa tena baada ya maandamano.

Mkuu wa polisi, Kale Kayihura, amesema maandamano hayo sio halali, na yeyote atakayeshiriki katika maandamano hayo atakamatwa.