Mutai ashinda London Marathon

Emmanuel Mutai amevunja rekodi na kuibuka mshindi wa London Marathon huku mwenzake Mary Keitani pia akishika nafasi ya kwanza katika mashindano ya wanawake.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Emmmanuel Mutai

Mutai alivunja rekodi kwa kukimbia kwa saa 2:04:39 na Keitany alichukua ushindi kwa saa mbili, dakika 19 na sekunde 17.

Katika mashindano ya wanaume, Martin Lel alichukua nafasi ya pili, huku mwenzake kutoka Kenya, Patrick Makau, akimaliza katika nafasi ya tatu.

Wakenya walitwaa ubingwa kwa kuchukua nafasi zote tatu za kwanza katika mashindano hayo.

Bingwa mtetezi katika mashindano ya wanawake, Liliya Shobukhova kutoka Urusi, alichukua nafasi ya pili.

Image caption Ketiany, wa tatu kushoto

Keitany ambaye anashiriki katika mashindano haya kwa mara ya pili alionekana kudhibiti mkondo wa mwisho wa mbio hizo na kumshinda Shobukhova kwa karibu dakika moja.

Shobukhova alionekana kushabikiwa sana kuwa atashikilia ubingwa wake wa London Marathon na alikuwa akiongoza mwanzoni mwa mashindano hayo, lakini Keitany aliongeza kasi alipofika maili 15 na kuendelea hivyo hadi tamati.

Edna Kiplagat mwenye umri wa miaka 31 alichukua nafasi ya tatu na hii ni mara yake ya kwanza kushiriki katika mashindano haya ya riadha ya London Marathon.

Keitany alianza riadha mwaka 2007 kama mchochea kasi na aliibuka mwanamke wa 10 kukimbia kwa muda wa saa mbili na dakika 20.

Mwanariadha huyo sasa ana nafasi nzuri ya kushiriki katika Olympic Marathon mwaka 2012.