Uasi Burkina Faso wasambaa

Jeshi la waasi lililoibuka wiki iliyopita Burkina Faso, taifa lililopo magharibi mwa Afrika limeenea mpaka mji mwengine wa nne.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Basi limechomwa moto Burkina Faso

Maandamano yameanza katika mji wa Kaya kaskazini mwa nchi hiyo, kufuatia ghasia mjini Po na Tenkodogo.

Ghasia hizo zimeanza Alhamis iliyopita wakati maaskari na walinzi wa rais kwenye mji mkuu wa Ouagadougou walipopinga kutopewa posho ya nyumba.

Saa chache kabla vurugu hazikuibuka, maelfu ya watu waliandamana kupinga gharama kubwa za bei ya vyakula.

'Polisi wajiunga na uasi'

Rais Blaise Compaore, aliyewahi kuongoza mapinduzi tangu mwaka 1987, ameifukuza serikali na kumteua kiongozi mpya kuwa mkuu wa majeshi kujaribu kutuliza ghasia.

Serikali yake ilitoa onyo siku ya Jumapili kuwa walioasi watakabiliwa na "sheria kali".

Mwandishi wa BBC mjini Ouagadougou Mathieu Bonkongou alithibitisha ghasia hizo kufika mpaka mjini Kaya.

Iliripotiwa kuwa maaskari na polisi waliingia mitaani siku ya Jumapili jioni na kuanza kufyatua risasi angani mpaka muda wa asubuhi wa Jumatatu.

Vurugu hizo kwenye mji mkuu zimesababisha takriban watu 45 kujeruhiwa na kulazwa hospitali.

Mwezi Machi, baadhi ya askari walighadhibika na kufanikiwa kuwaachia huru wenzao wengi ambao walifungwa kutokana na ubakaji.