Museveni aonya mataifa ya Magharibi

Rais Museveni wa Uganda amelaani hatua ya nchi za magharibi kuingilia kati masuala ya Afrika na kuonya kuwa jambo hilo watalivalia njuga.

Image caption Rais Yoweri Museveni

Bw Museveni pia amekanusha madai kuwa Muungano wa Afrika umeshindwa kushughulikia migogoro ya Afrika hususan suala la Libya.

Bw Museveni ameyasema hayo mwishoni mwa juma alipokutana na waandishi habari nyumbani kwake Rwakitura, magharibi mwa Uganda, ambapo amezungumzia masuala mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.

Mashambulizi

Hii ni mara ya kwanza kwa rais Museveni kukutana na waandishi wa habari wa Uganda na wa kimataifa, tangu achaguliwe tena kuliongoza. Amezungumzia masuala mbalimbali.

Alizungumzia suala la Libya - ambapo yeye ni rafiki wa Kanali Muammar Gaddafi - inayokabiliwa na upuinzani sio tu kutoka kwa raia wa mashariki mwa nchi lakini pia na mashambulizi ya anga ya Nato.

Bw Myuseveni alisema mashambulizi hayo ni hatua ya mataifa ya Ulaya kujiingiza katika masuala ya Afrika.

Ukoloni mamboleo

Alisema kuwa hii ni hatua mpya wakati huu japo walikuwa wanafanya hivyo wakati wa nyuma.

Ameongeza kuwa Afrika itaweza kushinda watu wanaotaka kuleta alichosema "ukoloni mamboleo kama ilivyofanya kupambana na ukoloni siku za nyuma".

Bw Museveni amesema mataifa ya magharibi yalifanya vibaya kutohusisha Muungano wa Afrika.

Ameonya

Mwandishi mmoja alipendekeza kuwa huenda uingiliaji huo wa mataifa ya magharibi ulichochewa na kujivuta kwa muungano wa Afrika.

Museveni alipinga hoja hiyo, akisema muungano wa Afrika umefanya mengi, kama vile kuipatia uhuru Afrika kusini, kumfukuza Idi Amin kutoka Uganda na pia suala la Libya na Ivory Coast.

Alisema muungano huo ungeweza kutatua suala la Libya.

Aidha ameonya kuwa ikiwa nchi za Ulaya hazitakoma kuingilia kati masula ya Afrika wajitayarishe kwa kile alichoita "Vietnam nyingine".