Mauaji ya Wagalla

Kenya
Image caption Ramani ya Kenya

Kwa kipindi kirefu koo za Ajuran na Degodia kutoka jamii ya wasomali wamekuwa wakizozana, kuhusu masuala tofuati ikiwemo malisho na maji ya mifugo.

Wakati wa makabiliano hayo silaha nzito nzito zilikuwa zikitumika.

Hali ambayo ilitatiza serikali ya Rais Daniel arap Moi wakati huo, kutokana na utovu wa usalama katika eneo hilo la kaskazini mwa Kenya kwenye mpaka na Somalia.

Silaha haramu

Kufuatia hali hiyo serikali ilianzisha mikakati ya kuwapokonya raia silaha katika eneo hilo la Wajir. Jamii ya Ajuran walitii amri lakini wenzao wa Degodia wakakaidi.

Wiki hiyo ilioanza Februari tarehe 10 mwaka 1984, vikosi vya usalama likiwemo jeshi, viliingia wilaya ya Wajir kufuatia shambulio kwenye kijiji kimoja. Kwenye harakati hizo za kutafuta silaha haramu, wanaume, vijana na wanawake wengine wakiwa wamebeba watoto wao mgongoni, walitiwa nguvuni na kusafirishwa kwenye malori ya jeshi hadi kwenye uwanja wa Wagalla.

Kulala uchi

Wakiwa kwenye uwanja wa ndege wa Wagalla, baada ya kukataa au kushindwa kuwaelekeza maafisa wa uslama palipo silaha. Mateso yalianza. Waume na wake waliamrishwa kuvua nguo na kulala uchi kwenye uwanja huo.

Walitembezewa kichapo kwa kipindi cha siku tano, bila chakula wala maji licha ya viwango vya joto kuwa juu kupita kiasi cha kawaida. Walionusurika walilazimka kunywa mikojo yao.

Mateso yalipozidi baadhi walijaribu kutoroka ndipo wakapigwa risasi. Miili ya waliouawa ikatupwa kwenye msitu, ili iliwe na wanyama pori, kulingana na wakaazi wa Wajir lengo lilikuwa kuficha ushahidi wa tukio hilo.

Msamaha

Kufikia leo hakuna aliyehusika amechukuliwa hatua na wala haijulikani aliyetoa amri maafa hayo yatendeke. Je rais ndiye aliyeamrisha au ulikuwa uamuzi wa wakuu wa usalama waliokuwa na hamaki ya kuonyesha wamefanya kazi?

Jibu hilo ndio tume hii ya haki na maridhiano inajukumu la kutafuta, baada ya hapo ipendekeze msamaha kwa wale watakao kiri makosa waliotenda au kufunguliwa mashataka kwa wale itakaopata ushaidi wa kutosha dhidi yao.