Fabregas: Arsenal inakosa ari ya ushindi

Nahodha wa Arsenal Cesc Fabregas amesema kukosekana kwa ari ya ushindi kumesababisha klabu hiyo kukosa vikombe tangu mwaka 2005.

Image caption Nahodha wa Arsenal Cesc Fabregas

Fabregas pia anaamini meneja Arsene Wenger kama angekuwa anafundisha soka Hispania, huenda angekwishafukuzwa kazi.

"Kwangu mimi, tunakosa ari ya ushindi, pia kukomaa katika kukabiliana na hali ngumu. Tunao wachezaji wengi wenye vipaji, lakini wanakosa kujiamini," alisema.

Arsenal inakabiliana na Tottenham siku ya Jumatano katika mchezo ambao utaamua hatma yao ya kuweka hai tamaa ya kubeba ubingwa msimu huu wa Ligi Kuu ya England.

Matokeo yoyote zaidi ya ushindi kwa kikosi cha Wenger katika uwanja wa White Hart Lane, kutathibitisha mbio za kunyakuwa kombe zitakuwa zimefikia ukingoni kwa msimu wa sita mfululilizo.

Fabregas amelieleza gazeti la Hispania la Don Balon: "Kuanzia mwaka 2007 nilikwishaanza kusema hatushindi, lakini tunacheza vizuri. Na sasa unashuhudia ukweli.

"Tatizo ni kwamba timu inahitaji kushinda kitu na ndio maana ilikuwa muhimu kushinda mchezo wa fainali ya Kombe la Carling, pale tulipofungwa 2-1 na Birmingham katika mchezo wa fainali.

"Unatakiwa uamue: ama ucheze na ushinde, au ukuze wachezaji."

Na Fabregas anaamini meneja wa Arsenal, Wenger angekabiliwa na chagizo kubwa nchini Hispania ili alete kikombe.