Ufaransa kutuma maofisa Libya

Ufaransa imethibitisha kuwa inatuma idadi ndogo ya maofisa wake wa ushauri wa kijeshi kushirikiana na waasi wanaompinga Kanali Gaddafi nchini Libya. Hapo jana Uingereza ilisema kuwa inatuma kikundi cha wataalamu wa masuala ya kijeshi huko mashariki mwa nchi mjini Benghazi kutoa mafunzo na mpangilio wa mafunzo ya kijeshi.

Bila shaka huu ni mpango ulioandaliwa na serikali za nchi hizo mbili. Ufaransa sasa imethibitisha kuwa kama Uingereza inatuma kikundi kidogo cha wataalamu wa kijeshi nchini Libya wasaidie kuwafunza waasi mbinu za kijeshi.

Kwa mujibu wa msemaji wa serikali Francois Baroin, idadi ya washauri hao haizidi watu kumi sawa na kikundi cha Uingereza, lengo lao ni kuwadokezea juu ya mpangilio wa jeshi, usimamizi wa ugavi wa askari na mawasiliano baina yao upungufu uliojitokeza.

Mara tena Bw.Baroin alirudia kauli ya serikali ya Uingereza kwamba bila shaka wanajeshi wa Ufaransa hawatoshiriki mapigano.

Hilo aliongezea ni kukiuka azimio la Umoja wa Mataifa namba 1973 ingawa kutuma kikundi cha wataalamu kutaonekana kuzingatia kifungu cha azimio hilo cha kulinda maisha ya wananchi wa Libya.

Kama ilivyo nchini Ufaransa, nchini Uingereza kuna wanaohoji kampeni inayofanywa nchini Libya ambayo inaweza ikageuka na kuwa jukumu la kudumu ikibainika kuwa serikali hizi mbili zinazidi kulishinikiza azimio la Umoja wa Mataifa hadi kikomo chake katika juhudi zao za kuona waasi wakifaidi zaidi.