Uingereza kusaidia wanajeshi wa waasi Libya

Wanajeshi wa Waasi Nchini Libya Haki miliki ya picha AP
Image caption Wanajeshi wa Waasi Nchini Libya

Libya imeghadhabishwa na tangazo la Uingereza, kuwa itatuma maafisa wa kijeshi kutoa ushauri wa kiufundi kwa waasi katika mji wa Benghazi unaodhibitiwa na upinzani.

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Libya, Abdelati Al-Obeidi, ameambia BBC kuwa hatua hiyo itaathiri vibaya juhudi za amani na kuendeleza uhasama uliopo.

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Uingereza, William Hague, alisema kuwa maafisa hao wa kijeshi wa Uingereza, hawatahusika katika kutoa mafunzo ya kijeshi au kuwapa silaha wapinzani wa Kanali Gaddafi, lakini watatoa ushauri kuhusu jinsi ya kuimarisha jeshi lao na njia ya mawasiliano.

Uingereza inasema itatuma washauri kumi na wawili wa kijeshi watakaosaidia wapinzani wa Kanali Gadaffi, kwa kutoa mwongozo, mpangilio, mawasiliano na kusambaza misaada kwa raia.

Hatua hii imekosolewa vikali na baadhi ya watu wanaoiona kuwa njama dhidi ya serikali ya Libya.

Wengine wamefananisha hatua hiyo ya Uingereza na uamuzi wa Marekani, wa kuingilia mzozo wa Somalia katika miaka ya tisini.

Mwanzoni, Marekani ilisema inafanya operesheni ya kutoa misaada kwa raia lakini baada ya muda wanajeshi hao walikabiliana na wale wa Somalia kwenye mitaa ya Mogadishu.

Machoni mwa umma, Uingereza inasisitiza kuwa shughuli hii itasaidia hasa katika kutoa misaada nchini Libya lakini malengo ya Uingereza na mataifa mengine hayajabadilika, kumuondoa madarakani Kanali Muammar Gadaffi.