Haye na Klitschko kutwangana Julai pili

Mpambano wa ubingwa wa ndondi za uzito wa juu duniani kati ya David Haye na Wladimir Klitschko, sasa utafanyika tarehe 2 mwezi wa Julai, mjini Hamburg, kwa mujibu wa meneja wa Klitschko, Bernd Boente.

Image caption Klitschko na Haye

Baada ya mazungumzo ya kina awali Haye bingwa wa uzito wa juu wa WBA na bingwa wa IBF na WBO Klitschko, walikubaliana kutwangana katika tarehe na sehemu ambayo haikupangwa.

Lakini Boente amethibitisha ukumbi unaoingiza watazamaji 57,000 wa Imtech Arena nchini Ujerumani ndipo makonde ya miamba hao yatakapovurumishwa.

"Pambano litakuwa tarehe 2 mwezi wa Julai mjini Hamburg. Hili nathibitisha kwa asilimia 100," alisema Boente.

"Tulikuwa na mtazamo tofauti na tumefanya mazungumzo kwa nchi nyingine. Switzerland ilikuwa moja wapo, Ukraine na sehemu nyingine za Ujerumani pia zilifikiriwa.

"Lakini mara zote alikuwa ni meneja wa Haye, Adam Booth pamoja na mimi, tuliyezungumzia masuala hayo, kama vile muelekeo tofauti wa kibiashara na baadae tukaamua kwa mpambano huo ufanyike Hamburg."

Haye awali alipangwa kupambana na Wladimir, mwenye umri wa miaka 35, mwaka 2009 lakini alilazimika kujiondoa kwa sababu ya kuumia mgongo na mara zote mazungumzo ya kufanyika pambano hilo yamekuwa yakikwama.

Klitschko amekuwa katika matibabu baada ya kuumia tumboni mwezi wa Desemba - kuumia ambako kulivuruga mipango ya pambano baina yake na Muingereza mwengine Dereck Chisora.

Haye, mwenye umri wa miaka 30, ambaye kwa sasa anafanya mazoezi ya kujiandaa mjini Miami, ana matumaini baada ya kumalizana na Wladimir achakazane na kaka yeke Wladimir, ambaye ni bingwa wa WBC Vitali Klitschko.

Hata hivyo, Haye mwenye maskani yake jijini London, amesema hatavuruga mipango yake ya kustaafu atakapofikisha umri wa miaka 31 mwezi wa Oktoba, akiwa amekamilishan ndoto ya kuwatwanga ndugu hao wawili.