Mpinzani Nigeria apinga matokeo

Haki miliki ya picha AP
Image caption Hoteli iliyopigwa bomu Kaduna

Mpinzani mkuu katika uchaguzi wa urais Nigeria, Jenerali Muhammadu Buhari, amesema kulikuwa na hila iliofanywa kwenye uchaguzi wa Jumamosi.

Bw Buhari ambaye aliwahi kuwa mkuu wa majeshi aliiambia redio ya Marekani kuwa kuna maeneo upande wa kusini wenye wafuasi wake wengi hawakuruhusiwa kupiga kura.

Lakini alisema chama chake kitapinga matokeo kwa mujibu wa sheria na kusihi kuwepo kwa amani baada ya ghasia kuibuka upande wa kaskazini kufuatia Goodluck Jonathan, aliyetoka kusini, kushinda.

Shirika la msalaba mwekundu limesema watu 48,000 kwa sasa wamekimbia vurugu hizo.

Katika jimbo la Kaduna, vyanzo vya polisi vimeiambia BBC takriban watu 400 wamekamatwa wakihusishwa na mapigano hayo.

Mwandishi wa BBC Abdullahi Kaura Abubakar amesema kwa sasa hali imetulia kwenye mji wa Kaduna, ambapo mitaa imejaa maiti zilizochomwa moto na wengine wakachoma makanisa, vituo vya polisi pamoja na nyumba baada ya siku mbili za ghasia.

Alisema, mapigano yanaendelea katika maeneo mengine ya jimbo hilo na majeshi ya usalama yamesambazwa zaidi maeneo hayo.

Bw Jonathan alitangazwa kuwa mshindi kwenye uchaguzi wa rais siku ya Jumamosi, huku tume ya uchaguzi ikisema kapata takriban asilimia 57 ya kura zote ambayo ni kura milioni 22.5 ukilinganisha na kura milioni 12.2 za Bw Buhari.

Waangalizi wa kimataifa walisema uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki.