Man United yazidi kujichimbia kileleni

Javier Hernandez ama Chicharito alifunga bao pekee dakika za mwisho na kuiwezesha Manchester United kuzidi kuongoza Ligi Kuu ya England kwa pointi tisa, katika mchezo mkali dhidi ya Everton.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Chicharito baada ya kufunga bao pekee la Manchester United

Sylvain Distin alishindwa kumiliki mpira na Everton wakalipa uzembe huo, zikisalia dakika saba kabla mchezo haujamalizika, kwa Chicharito kuudonoa kwa kichwa mpira wa krosi uliochongwa na Antonio Valencia kando mwa mlingoti wa lango.

Hernandez mapema alipoteza nafasi mbili nzuri baada ya mlinda mlango wa Everton, Tim Howard kuzuia mikwaju yake kwa ustadi.

Manchester United kwa sasa inahitaji pointi saba tu katika mechi zake nne zilizosalia ili wajihakikishei ubingwa wa Ligi Kuu ya soka ya England kwa mara ya 19.

Katika mchezo mwingine Maxi Rodriguez aliweza kufunga mabao matatu, Liverpool ilipojibidiisha kutafuta nafasi ya kucheza Ligi ya Europa kwa kuiadhibu Birmingham mabao 5-0 katika uwanja wa Anfield.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Maxi akishangilia moja ya mabao yake matatu kwa Liverpool

Mabao mengine ya Liverpool yaliwekwa wavuni na Dirk Kuyt na Joe Cole.

Ushindi huo wa Liverpool umeiweka katika nafasi ya sita wakiwa na pointi 52.

Sunderland nayo ikicheza soka ya kuvutia katika kipindi cha pili ilifanikiwa kuizamisha Wigan mabao 4-2 na kujipatia ushindi wake wa kwanza katika mechi 10 zilizopita.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Asamoha Gyan

Mabao ya Sunderland yaliwekwa wavuni na Gyan Asamoha, Henderson, Sessegnon kwa mkwaju wa penalti na Henderson, wakati Wigan waliokuwa wa kwanza kufunga, mabao yao yalifungwa na Diame na 52 Di Santo.

Matokeo hayo hayo yameipatia Sunderland pointi 41 kuiweka nafasi ya 10, huku Wigan iliyojikwamua kutoka eneo la kushuka daraja wiki mbili zilizopita, sasa imerejea katika nafasi ya chini ya 18.

   Matumaini ya Tottenham kucheza katika Ligi ya Ubingwa kwa vilabu vya Ulaya, yaliingia dosari baada ya kulazimishwa sare ya 2-2 katika uwanja wao wa nyumabni walipocheza na West Brom.

   Haki miliki ya picha Getty Images
   Image caption Roman Pavlyuchenko

   Westa Brom walikuwa wa kwanza kulifungua lango la Spurs mapema dakika ya tano kwa bao la Peter Odemwingie, kabla ya Pavluchenko kusawazisha na Tottenhama wakaongeza bao la pili lililofungwa na Jarmin Defoe, kabla ya West Brom kusawazisha kwa bao la Cox.

   Matokeo hayo yameibakiza Tottenham katika nafasi ya tano na pointi 55. West Brom wamekusanya pointi 40 na kuondoa wasiwasi wa lile kundi la kushuka daraja.

   Sare nyingine ya bao 1-1 zilitawala mchezo kati ya Aston Villa na Stoke, Blackpool na Newcastle na pia Wolves na Fulham.