Misri kuchuana U20 Kombe la Dunia

Misri wamefaulu kushiriki katika michuano ya ubingwa wa Afrika kwa timu za vijana, baada ya kuilaza Afrika Kusini 1-0 Jumamosi.

Image caption Timu ya Misri waliposhinda Kombe la Mataifa ya Afrika 2010

Matokeo ya mechi hiyo imeipa timu hiyo ya Young Paharaohs nafasi ya kuchuana katika Kombe la Dunia la vijana chini ya umri wa miaka 20, litakalofanyika Columbia mwezi Julai.

Timu hiyo ya Afrika Kaskazini walifunga bao wakati wa dakika za mwisho, nusu ya kwanza ya mchezo, na kuibuka washindi na nafasi ya pili katika kundi la A.

Mohamed Hamdy Zaky alitumia pengo lililoachwa na kipa Hayden Williams na kuipa Misri ushindi.

Timu ya Mali ndio bingwa katika kundi hilo baada ya kusawazisha 1-1 na Lesotho.

Kiungo wa Young Eagles Drissa Ballow alifunga bao dakika ya 17 lakini Christopher Boseka Mosiuda wa Lesotho alifunga bao katika dakika ya 82.

Mali ilichukua nafasi ya kwanza katika kundi hilo na pointi 7 huku Misri ikifuata na pointi 6.

Afrika Kusini ilichukua nafasi ya tatu na Lesotho nafasi ya nne, hivyo basi timu zote mbili zimepoteza nafasi ya kuendelea.

Misri itachuana na washindi kutoka kundi la B katika nusu fainali, nayo Mali itachuana na timu iliyochukua nafasi ya pili kutoka kundi hilo la B pia.