Mji wa Deraa, Syria, bado umekaliwa

Inaarifiwa kuwa jeshi la Syria linaendelea kukandamiza maandamano katika mji wa kusini wa Deraa ambao tangu Jumatatu umekaliwa na wanajeshi na vifaru.

Haki miliki ya picha Reuters

Risasi zimesikika katika mji huo wa kale, na walioshuhudia matukio ya huko, wanasema kumetokea mapambano karibu na msikiti mkuu wa Deraa.

Waandishi wa habari kutoka nchi za nje hawaruhusiwi nchini Syria na haijulikani wazi kinachotokea nchini humo.

Katika miji kadha, familia za wale waandamanaji waliouwawa Ijumaa, zinatarajiwa kuwazika hii leo.

Wanaharakati wanaopigania haki za kibinaadamu wanasema waandamanaji zaidi ya 60 waliuwawa kwenye maandamano katika sehemu mbali mbali za Syria; zaidi ya nusu waliuwawa mjini Deraa.

Serikali inasema idadi ya waliouwawa ni ndogo sana, na kwamba wanajeshi nao piya walikufa.