Berbatov kutocheza Jumanne na Schalke 04

Manchester United itamkosa mpachika mabao wake hodari Dimitar Berbatov kwa mechi ya kwanza ya nusu fainali siku ya Jumanne wa Ligi ya Ubingwa wa Ulaya dhidi ya Schalke 04 ya Ujerumani.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Dimitar Berbatov

Berbatov bado anasumbuliwa na maumivu ya nyonga hali iliyosababisha asicheze mchezo wa siku ya Jumamosi wa Ligi dhidi ya Everton.

Mshambuliaji huyo ana nafasi ndogo kucheza dhidi ya Schlake 04, na kukosekana kwake kutaikosesha Manchester United mfungaji muhimu iwapo watafanya mabadiliko.

Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson amesema kwa sasa hana majeruhi mpya katika orodha ya wachezaji wake kabla ya pambano hilo na Schalke 04 siku ya Jumanne katika uwanja wa Veltins-Arena.

Nahodha na mlinzi wa kati Nemanja Vidic na kiungo Park Ji-Sung walipumzishwa katika mchezo wa siku ya Jumamosi na watacheza dhidi ya Schalke.

Mlinzi wa pembeni kushoto Patrice Evra na kiungo Michael Carrick walikuwa ni miongoni mwa wachezaji waliobadilishwa katika mchezo dhidi ya Everton uliofanyika Old Trafford.

Ryan Giggs pia aliingia akiwa mchezaji wa akiba dhidi ya Everton na hapana shaka yoyote ataanza katika mchezo huo wa Ubingwa wa Ulaya, hali itakayomfanya kuwa mchezaji pekee mwenye uzoefu mkubwa wa mikikimikii ya mashindano ya Ulaya.