Mabomu yalipuka Nigeria

Image caption Milipuko ya mabomu Nigeria

Mabomu matatu yamelipuka mjini Maiduguri kaskazini-mashariki mwa Nigeria, na kuua takriban watu watatu.

Mabomu mawili yalilipuka kwenye hoteli na jengine kwenye kituo cha usafirishaji siku ya Jumapili usiku.

Polisi wamesema walioathirika wamepelekwa kwenye hospitali mbili tofauti mjini humo.

Kundi la kiislamu la Boko Haram linalopinga vitabu vya magharibi limelaumiwa kwa mashambulio kama hayo ambalo limekuwa likipambana na majeshi ya usalama mjini hapo.

Milipuko ya hivi karibuni imetokea kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa magavana siku ya Jumanne katika majimbo 36 ya Nigeria.

Ghasia ziliibuka kaskazini mwa Nigeria kufuatia uchaguzi wa rais Aprili 16, ambapo Bw Goodluck Jonathan aliyetoka upande wa kusini aliibuka mshindi.

Mamia wanaaminiwa kuuawa na maelfu wamekimbia makazi yao.

Haikufahamika iwapo milipuko hiyo ya mabomu mjini Maiduguri, mji mkuu wa jimbo la Borno, lina uhusiano wowote na ghasia hizo.