United yaichapa Schalke 2-0

Manchester United imepiga hatua kubwa kuelekea katika fainali ya Klabu Bingwa Ulaya, baada ya kuifunga Schalke katika nusu fainali ya kwanza nchini Ujerumani.

Image caption Giggs amekuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kufunga goli katika michuano hii

United wangeweza kufunga mabao mengi kabla ya mapumziko, kama sio uhodari wa kipa wa Schalke, Manuel Neuer.

Hata hivyo United walipata bao la kwanza katika kipindi cha pili, baada ya Wayne Rooney kupenyeza pasi wa Ryan Giggs. Rooney baadaye alipachika bao la pili baada ya kupata pasi kutoka kwa Javier Hernandez.

United itaikaribisha Schalke kwenye uwanja wa Old Trafford, Jumatano tarehe 4 mwezi Mei, kwa ajili ya mchezo wa pili wa nusu fainali.

Iwapo watadhibiti ushindi wao, United itawakilisha soka ya England katika Fainali ya Klabu Bingwa Ulaya itakayochezwa kwenye uwanja wa Wembley.