Mancini afurahia bao la kwanza la Dzeko

Meneja wa Manchester City Roberto Mancini, amefurahishwa na bao lililofungwa na Edin Dzeko baada ya mshambuliaji huyo kufunga bao lake la kwanza la Ligi Kuu ya England wakati Man City walipoilaza Blackburn bao 1-0.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Edin Dzeko akishangilia bao lake dhidi ya Blackburn

Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Bosnian alijiunga na Manchester City, akitokea Wolfsburg mwezi wa Januari kwa kitita cha paundi za Uingereza milioni 27 na awali alishawahi kufunga mabao mawili katika mchezo wa kugombea Kombe la FA na Ligi ya Europa.

Lakini baada ya kucheza mechi tisa za ligi pasi na kufunga, hatimaye Dzeko aliuona mlango.

"Nimefurahishwa sana na Edin kwa sababu alistahili kufunga bao, ni mchezaji mzuri na ni mtu mzuri," alisema Mancini.

"Nina hakika itasaidia kumjengea imani. Edin ni mshambuliaji mzuri sana.

"Alikuwa na matatizo kwa kutocheza baadhi ya mechi na alikuwa akikabiliwa na shida ya kufunga, lakini usiku huu amefunga bao muhimu kwetu.

"Haikuwa rahisi kwake kwa hiyo nimefurahi.

"Huku Carlos Tevez akiwa majeruhi, Mario Balotelli alicheza kandanda safi na wakati huu Edin ameweza kufunga bao lake la kwanza la ligi ni jambo muhimu."

Ukame wa kufunga mabao kwa Dzeko ulikuwa unalinganishwa na wa Fernando Torres, aliyejiunga na Chelsea akitokea Liverpool kwa kitita cha paundi milioni 50 mwezi wa Januari, lakini alifunga bao lake la kwanza dhidi ya West Ham siku ya Jumamosi.

Dzeko, mwenye umri wa miaka 25, alisema: "Hii ni kandanda, Torres alifunga mabao mengi alipokuwa Liverpool na akabadili klabu, ninampongeza kwa sababu nafahamu chagizo mchezaji inayokukabili.

"Sasa inatulazimu kuangalia mbele - leo mambo yalikuwa mazuri, ni mwanzo mpya kwangu na kwa Man City.

"Ninafurahi hili bao limeisaidia timu yangu kushinda mchezo.

"Baadhi ya nyakati inakuwa vigumu, mimi si wa kwanza kuwa na mwanzo mgumu, lakini ninafuraha kwa sababu nimefunga bao leo na limeisaidia timu."

Matokeo hayo yameipeleka Manchester City pointi nne dhidi ya wanaoshika nafasi ya tano Tottenham na timu zote mbili zimesaliwa na michezo mitano zikipigania kucheza Ligi ya Mabingwa wa Vilabu vya Ulaya msimu ujao.