Obama aomboleza maafa ya Alabama

Alabama Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Mamia ya watu wamefariki baada ya vimbunga vikali kupiga kusini mwa Marekani

Rais Barack Obama amesema serikali yake itafanya kila juhudi kusaidia wakaazi wa jimbo la Alabama kufuatia athari za dhoruba kali na kimbunga.

Zaidi ya watu 280 wameuawa na uharibifu mkubwa umefanyika katika jimbo hilo la kusini mwa Marekani.

Serikali imetangaza hali ya hatari katika eneo hilo ambako watu wamelazimika kuondoka kwenye makaazi yao.

Maafa na uharibifu pia yametokea katika majimbo ya Tennessee, Mississippi, Georgia na Virginia.

Rais Obama amesema ataelekea Alabama kuugana na familia za walioathirika na makundi yanayotoa misaada ya dharura kwa wakaazi wa eneo hilo.

Shirika la kitaifa la kutabiri hali ya hewa nchini Marekani, limesema eneo hilo la kusini mwa marekani limepigwa na msururu wa vimbunga 300 tangu ijumaa wiki iliopita. Vimbunga venye nguvu zaidi vilipiga jumatano wiki hii.

Kufikia jana zaidi ya watu milioni moja walikuwa hawana huduma za umeme.

Wanajeshi 2,000 wametumwa kusaidia katika harakati za uokozi.