Israel inazuwia kodi ya WaPalestina

Israel imesimamisha malipo ya kodi za foridha inazokabidhi kwa Utawala wa Kipalestina, baada ya kutangazwa juma lilopita, kwamba makundi mawili ya Wapalestina yaliyokuwa yakipingana, Fatah na Hamas, yanaungana.

Waziri wa Fedha wa Israel, Yuval Steinitz, alisema anazuwia malipo ya ushuru na kodi nyengine zinazotozwa na Israel kwa niaba ya Utawala wa WaPalestina, hadi itapojulikana wazi, kuwa fedha hizo hazitowafikia wapiganaji wa Hamas.

Jumla ya fedha hizo ni karibu dola milioni 90.

Israel inaichukulia Hamas, inayodhibiti eneo la Gaza, kuwa kikundi cha magaidi.

Shughuli za kukusanya ushuru kwa niaba ya Wapalestina ni kati ya makubaliano ya muda ya amani, baina ya Israel na chama cha Fatah cha Rais wa Wapalestina, Mahmoud Abbas.

Na waziri mdogo wa Israel, Silvan Shalom, anasema, tangazo la Misri kwamba inapanga kufungua kituo cha Rafah, kwenye mpaka wa Misri na Gaza, ni jambo linalotia wasi wasi.

Akizungumza kwenye televisheni ya Israel, Bwana Shalom alionya, kwamba kufunguliwa kwa kituo hicho kunaweza kupelekea silaha na magaidi kuingia Gaza, ambayo inadhibitiwa na wapiganaji wa Kiislamu wa Hamas.

Alisema Israel lazima ijitayarishe kwa mabadiliko makubwa yatayotokea Misri na sehemu nyengine za Mashariki ya Kati, baada ya mtibuko wa siasa katika kanda hiyo.