Besigye akwama katika uwanja wa ndege Nairobi

Dr. Kizza Besigye akizuiliwa na polisi Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Dr. Kizza Besigye akizuiliwa na polisi

Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye, amekwama katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta Mjini Nairobi, baada ya maafisa wa shirika la ndege la Kenya, Kenya Airways, kumzuia kupanda ndege.

Kiongozi huyo alikuwa akirejea nyumbani baada ya kupokea matibabu katika hospitali moja mjini Nairobi, kufuatia majeraha aliyoyapata wakati alipokamatwa na polisi wiki mbili zilizopita mjini Kampala.

Akiongea na BBC Dr. Besigye, amesema kuwa alifahamishwa na maafisa wa shirika hilo la ndege kuwa wameonywa wa serikali ya Uganda.'' wamenifahamisha kuwa serikali ya Uganda, imewaonya kuwa ndege hiyo haitaruhusiwa kutua ikiwa watamruhusu kama abiria. Sasa tunataka shirika la ndege la Kenya Airways ambayo ilikuwa na wajibu wa kuturudisha nyumbani, kuelezea rasmi sababu za kuzuiliwa kwao''

Mwandishi wa BBC mjini Kampala anasema, kurejea kwa Dr Besigye, siku moja kabla ya kuapishwa kwa rais Yoweri Museveni, kunatishia kuharibia sifa serikali ya nchi hiyo.