Mabomu mawili 'yaua 69' Pakistan

Mashambulio mawili ya bomu katika kituo cha mafunzo ya kijeshi kaskazini magharibi mwa Pakistan yamesabaihsa vifo vya watu 69, polisi wanasema.

Image caption Shambulio la Bomu nchini Pakistan

Watu kadhaa walijeruhiwa katika shambulio kwenye kituo cha mafunzo ya kijeshi cha Shabqadar,wilaya ya Charsadda.

Kuna taarifa kuwa walipuaji wawili walitekeleza mashambulio hayo.

Ni shambulio baya zaidi kuwahi kutokea tangu vikosi vya Marekani vilipomuua kiongozi wa al-Qaeda Osama Bin Laden katika mji wa Abbottabad, kaskazini mwa Pakistan, tarehe mbili mwezi Mei.

Makundi ya wanamgambo yameapa kulipiza kisasi kwa kifo cha Bin Laden. Hata hivyo,kufikia sasa hakuna kundi limetangaza kuhusika na shambulio la Ijumaa.

"kulikuwa na milipuko miwili ya mabomu," Jahanzeb Khan,afisa mkuu wa polisi eneo la Shabqadar,ameambia shirika la habari la AFP.

Shambulio hilo lilitokea wakati makurutu wapya walipokuwa wanaingia kwenye mabasi kwa likizo fupi baada ya mafunzo,taarifa zinasema.

Magari kadhaa yaliharibiwa kutokana na shambulio hilo.