UN yaamrisha jeshi la Sudan kuondoka Abyei

Moto ukiwaka katika mji wa Abyei
Image caption Moto ukiwaka katika mji wa Abyei

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeitaka jeshi la utawala wa Khartoum nchini Sudan kuondoka katika jimbo la Abyei.

Jeshi hilo lilitwaa mji wa Abyei hapo Jumamosi ambapo majeshi ya utawala wa Kusini yaliondoka baada ya mapigano makali.

Shambulizi hili limetokea wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa ziarani Sudan. Baraza hilo limelaani mapigano hayo ya Abyei.

Mjumbe maalum wa Marekani nchini Sudan Pricenton Lyman amesema kitendo cha jeshi la Kharoum ni hatari kwa usalama wa taifa.

Image caption Nyumba zilizoharibiwa Abyei

Kwa upande wake Serikali ya Sudan kusini imesema kutwaaliwa na jimbo la Abyei ni tangazo la vita. Barnaba Marial waziri wa mawasiliano Sudan Kusini amelaumu Khartoum kwa kutatua matatizo yake kwa kutumia vujo.

Shirika la kutoa misaada la MSF limesema zaidi ya watu elfu 20 wamekimbia mwakao.

Kwa sasa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linatarajia kufanya ziara rasmi kusini mwa nchi ambapo litazuru maeneo ya Wau na Juba.

mapigano ya Abyei yamezidisha taharuki wakati Sudan Kusini ikijitayarisha kujitenga na kaskazini katika miezi michache ijayo.