Ocampo kushtaki vigogo wa Libya

Mwanasheria mkuu wa mahakama ya kimataifa kuhusu makosa ya jinai amesema kuna sababu za msingi kuwafungulia mashtaka askari wa vikosi vinavyomtii Kanali Mummar Gaddafi kwa uhalifu walioutenda dhidi ya raia wa Libya.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Moreno Ocampo

Katika taarifa yake, Luis Moreno Ocampo amesema kuwa kati ya mashtaka yanayoweza kufunguliwa ni kwa mauwaji, vifungo bila hatia, kunyanyasa na kuhukumiwa kifo.

Bw.Ocampo amesema mauwaji ya raia wanaoandamana kwa amani yanayofanywa na vikosi vya usalama kumekuepo na kufanywa kwa mipango.

Kanali Gaddafi amepambana na upinzania ulioanza miezi miwili sasa.

Mwanasheria mkuu huyo ambaye alipewa jukumu hilo na Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuchunguza madai ya vitendo vya kuwanyanyasa raia wa Libya, amedokezea kuwa kuna takwimu zinazokadiria hadi watu 500 hadi 700 waliuawa katika mwezi Febuari pekee.

'kuna vigogo wachache' Bw.Ocampo amesema kuwa anapanga kuwasilisha ombi lake la kwanza la kutaka waranti za kukamatwa kwa watu kadhaa katika siku chache zijazo.

WarrantI hizo zitagusa hasa matukio ya awali dhidi ya waandamanaji ingawa hazijabainisha ni nani atakayetajwa kufunguliwa mashtaka.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo madai ya visa hivi ni kwamba vilifanyika kutokana na amri iliyotolewa na watu wachache walio uongozini, ikiashiria kwamba huenda Kanali Gaddafi pamoja na kundi dogo la watu wake wa karibu wakafunguliwa mashtaka.

Bw.Ocampo amesema kuwa kuna ushahidi wa kutegemewa kwamba uhalifu wa kivita ulitendeka pindi hali ilipogeuka kuwa vita, akatowa mfano wa mashambulizi dhidi ya raia wasiokuwa na silaha pamoja na matumizi ya mabomu yanayotawanyika.

Afisi ya mwanasheria vilevile inaendelea kupeleleza pia madai kuhusu vitendo vya ubakaji, na habari kwamba makundi yaliyojaa ghadhabu katika mji wa Benghazi yaliuwa makumi ya watu weusi kutoka Mataifa ya Kiafrika kwa dhana tu kuwa ni mamluki.