Sheryl Cwele, afungwa miaka 12

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Bi Sheryl Cwele

Sheryl Cwele, mke wa waziri wa masuala ya kijasusi, amehukumiwa kifungo cha miaka 12 jela kwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Cwele, aliyeolewa na Siyabonga Cwele, alikuwa akiajiri wanawake kuingiza dawa hizo nchini Afrika kusini kutoka Uturuki na Marekani ya kusini.

Cwele alikutwa na hatia pamoja na mwenzake Frank Nabolisa, raia wa Nigera, katika mahakama kuu ya Pietermaritzburg.

Mshirika wake huyo Nabolisa naye amepewa hukumu hiyo hiyo ya miaka 12.

Madai ya biashara ya dawa za kulevya yalianza mwaka 2009 baada ya kukamatwa kwa mwanamke mmoja raia wa Afrika kusini aliyekamatwa Brazil na aina ya cocaine yenye thamani ya dola za kimarekani 300,000.

Tessa Beetge kwa sasa anatumikia kifungo cha miaka nane gerezani mjini Sao Paulo.

Alikutwa na kilo 10 za coaccaine kwenye mkoba wake.

Akitoa hukumu hiyo, Jaji Piet Koen alielezea makosa yao kuwa mazito mno.

Alisema, " Familia nyingi zinaathiriwa na dawa za kulevya zinazoletwa hapa kinyume cha sheria. Huteseka kutokana na wafanyabiashara wanaosababisha kutawaliwa na usambazaji wa mara kwa mara na kujikuta wakiwa wanaendela kutumia dawa hizo.

Watu hao wawili, ambao walikana mashtaka, walisema watakata rufaa dhidi ya hatia yao ya kufanya biashara hiyo.

Wangeweza kuhukumiwa kifungo cha miaka 15 jela.

Upinzani umetoa wito wa kumtaka Bw Cwele ajiuzulu, ukisema kama hajui shughuli za mkewe zilizo kinyume cha sheria, basi hana haja ya kuendelea kuongoza kitengo cha kijasusi nchini humo.