Ouattara wa Ivory Coast aapishwa

Alassane Ouattara anatarajiwa kuapishwa kuwa Rais wa Ivory Coast na mtu ambaye mwanzo alimkatalia ushindi wake katika uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi Novemba.

Mwezi Desemba, kiongozi wa baraza la katiba alimwidhinisha Laurent Gbagbo kuwa mshindi, iliyosababisha nafasi hiyo kushikiliwa naye kwa muda wa miezi minne.

Bw Gbagbo pia anatarajiwa kuhojiwa juu ya madai ya kukiuka haki za binadamu wakati akiwa madarakani.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Bw Alassane Ouattara

Hata hivyo, imeripotiwa kuwa mawakili wake kutoka Ufaransa wamenyimwa ruhusa ya kuingia Ivory Coast.

Shirika la habari la AFP limesema walizuiwa kwenye uwanja wa ndege wa Abidjan na kutiwa kwenye ndege iliyofuata na kurejeshwa Paris.

Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya unatarajiwa kuipa nchi hiyo msaada wa zaidi ya dola za kimarekani milioni 60.

Kamishna wa maendeleo wa Ulaya, Andris Piebalgs, ambaye yupo Ivory Coast, amesema inabidi waende kwa kasi.

Aliiambia BBC kuwa hali ilivyo nchini humo bado ina utata na kama maisha ya watu hayakuimarishwa haraka, ghasia zinaweza kuanza upya.

Alisema raia wa nchi hiyo wanahisi wamepoteza miaka 25 ya maendeleo kutokana na mapigano ya kisiasa na kikabila ya hivi karibuni.

Takriban watu 3,000 wanaaminiwa kuuawa wakati wa ghasia zilizotokea kwenye nchi inayozalisha kakao zaidi duniani, ambapo awali ilikuwa nchi yenye utajiri mkubwa Afrika magharibi.

Alipotokea

Alassane Ouatarra ni miongoni mwa kikundi kidogo cha watu ambao ni wasomi wa kisiasa nchini Ivory Coast, ambao harakati zao za kuwania madaraka zimeishia katika mapambano ya kupigania mji mkuu wa Abidjan mwezi uliopita.

Lakini mapambano hayo ya kuwania madaraka yalianza katika miaka ya mwanzo ya 1980.

Bw Ouatarra, ambae ni mtalamu wa uchumi aliyesomea Marekani, aliwahi kutumikia shirika la fedha la kimataifa IMF wakati huo na kwa muda mfupi aliteuliwa kuwa waziri mkuu.

Huo ndio ulikuwa mwanzo wa mchuano mkali kati ya Bw Ouatarra na watu wengine wawili.

Wote walikuwa vigogo kutoka chama kilichotawala wakati huo, Henri Konan Bedie, na Profesa wa Historia ambae wakati huu alijinasibu kuWa mwanaharakati wa kutetea demokrasia Laurent Gbagbo.

Silaha walizozitumia watu hao watatu katika vita vyao vya kisiasa zilikuwa ni asili yao ya mikoa ama makabila walikotoka na ushawishi wao wa kifedha.

Ni mwaka uliopita tu kwa msaada wa Umoja wa mataifa ndio kulianzishwa kitu kilichokaribia kuwa demokrasia ya vyama vingi.

Bw Ouatarra alishinda uchaguzi wa kwanza kabisa wa rais kwa njia ya mashindano wazi.

Lakini Bw Gbagbo, akipuuza madai yake ya kuwa mwanademokrasia alikataa kuachia madaraka.

Mapigano yaliyofuata yalisababisha zaidi ya watu 1,000 kuuawa, maelfu kupoteza makazi yao na kuangamiza uchumi wa taifa hili kuu la Afrika Magharibi.

Demokrasia ya Ivory Coast imekuja kwa gharama kubwa.

Alassane Ouatarra ameapishwa rasmi leo kuwa Rais wa Ivory Coast baada ya mgogoro wa kisiasa ulioifanya nchi hiyo kuingia katika vita.

Rais wa zamani Laurent Gbagbo alikataa kuachia madaraka baada ya kushindwa kwenye uchaguzi ulioshuhudiwa na ujumbe wa Umoja wa mataifa mwaka jana.

Gbagbo aliondolewa madarakani mwezi uliopita katika mapigano yaliyohusisha msaada wa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa na Ufaransa.