Sababu za kumfukuza balozi wa Uingereza

Rais wa Malawi Bingu wa Mutharika ameeleza sababu ya kumfukuza balozi wa Uingereza mwezi uliopita.

Image caption Bingu wa Mutharika

Katika taarifa yake ya mwanzo hadharani kuhusu ugomvi huo Rais Mutharika alisema Balozi Fergus Cochrane-Dyet alimtusi na hayuko tayari kukubali hayo eti kwasababu Malawi inapata msaada wake mkubwa kabisa kutoka Uingereza kushinda nchi nyengine.

Magazeti yalichapisha barua iliyofichuliwa ambamo Balozi Cochrane-Dyet alimuelezea Rais Mutharika kuwa anaongoza kimabavu na hakubali kukosolewa.

Uingereza ilimtaka balozi wa Malawi aondoke London kujibu kufukuzwa kwa Bwana Cochrane-Dyet kutoka Malawi.

Malawi ilimfukuza Cochrane-Dyet baada ya nyaraka za kisiri kufichuliwa ambazo zilikuwa zikitumwa kwa waziri wa mambo ya nje ya nchi wa Uingereza, William Hague, na kuwafikia waandishi habari.

Baada ya tukio hilo Ofisi ya mambo ya nje na jumuiya ya madola, FCO, mjini London ilimuamuru balozi wa Malawi Flossie Gomile-Chidyanga kuondoka Uingereza.

Uingereza hutuma paundi milionii 93 kwa Malawi kwenye mfuko wa msaada kwa nchi zinazooendelea na Malawi ni nchi inayopokea kiasi kikubwa cha msaada wa fedha.