Besigye kurudi Uganda

Bwana Besigye aliiambia BBC kwamba atarudi nyumbani na kuendelea kutembea kwa miguu hadi kazini kuonesha malalamiko juu ya kupanda kwa bei za bidhaa.

Image caption Kizza Besigye

Kiongozi wa upinzani wa Uganda, Kizza Besigye, alizungumza jana kutoka Kenya ambako amekuwa akitibiwa macho yaliyodhurika wakati askari wa usalama wa Uganda walipompulizia gesi ya pili-pili.

Bwana Besigye alisema hana budi kurudi Uganda.

Na mshauri wa rais katika mawasiliano na vyombo vya habari, John Nagenda, anasema ni salama kwa Bwana Besigye kurudi Uganda iwapo hatochochea ghasia.

"Hakika atakuwa salama. Lakini ikiwa ataendelea kufanya kama yale aliyofanya; na ameshawahi kusema kuwa ataifanya Uganda isiweze kuongozwa...ikiwa hiyo ndio azma yake, basi atazuwiwa", aliongeza.