Umoja wa mataifa waelezea hali ya wasiwasi Syria

Wapinzani wa serikali ya Syria mjini Deraa Haki miliki ya picha Other
Image caption Wapinzani wa serikali ya Syria mjini Deraa

Umoja wa Mataifa umeelezea wasi wasi kuhusu hali ya usalama katika mji wa Deraa Kusini mwa Syria, huku serikali ya nchi hiyo ikiendeleza mkakati wake wa kuwasaka wapiganaji wa waasi.

Umoja wa mataifa, umesema shirika lake la kutoa misaada, halijaruhusiwa kufika mjini humo na kuwa shirika lingine la kutoa misaada halijafanikiwa kupokea dawa na vifaa vya matibabu kuwasaidia wakimbizi wanaotoroka mapigano kati ya wanajeshi wa serikali na waasi.

Hakuna mawasiliano katika mji wa Deraa kwa muda wiki mbili sasa baada ya serikali ya nchi hiyo kutuma wanajeshi na vifaru ili kujaribu kutwaa udhibiti wa mji huo kutoka kwa wapiganaji wa waasi.

Wakati huo huo, muungano wa Ulaya EU umetangaza kuiwekea Syria marufuku ya kuagiza silaha.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa muungano huo, serikali ya nchi hiyo haitaruhusiwa kuagiza silaha au vifaa ambavyo vinaweza kutumiwa kukandamiza upinzani.

Maafisa 13 wa ngazi ya juu wa serikali ya Syria na washirika wao, pia wamepigwa marufuku kusafiri nchi 27 za muungano huo na amana zao zilizoko katika nchi za Ulaya zimezuiliwa.