Besigye aahirisha safari yake

Kiongozi wa upinzani wa Uganda Kizza Besigye ameiambia BBC kuwa sasa amerhusiwa kurejea nyumbani baada ya awali kusema alikuwa amezuiliwa.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Gari la Besigye likishambuliwa nchini Uganda

Mapema, alisema alizuiwa kupanda ndege kutoka Nairobi kwenda Uganda, baada ya kupatiwa matibabu nchini Kenya.

Serikali ya Uganda imekanusha kumzuia kusafiri.

Rais Yoweri Museveni aliyemshinda Dokta Besigye kwenye uchaguzi wa mwezi Februari, anatazamiwa kuapishwa siku ya Alhamisi.

Dk Besigye, ambaye anasema uchaguzi huo ulivurugwa, alikamatwa wakati wa maandamano nchini Uganda wiki mbili zilizopita, na macho yake kuumizwa kutokana na kupuliziwa maji ya pilipili.

Aliiambia BBC akiwa kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi: "Serikali ya Uganda imemuambia mkuu wa shirika la ndege la Kenya, kuwa iwapo wataniruhusu kusafiri ndege yao haitaruhusiwa kutua nchini Uganda, na hawakuwa na jinsi yoyote bali kutushusha."

Baadaye aliiambia BBC kuwa amepewa ruhusa kurejea lakini hakusema kwa nii mamlaka zimebadili mawazo.

Amesema mke wake amekuwa akizungumza na wafanyakazi wa shirika la ndege la Kenya katika ofisi zao jijini Nairobi.

Mwandishi wa BBC Anne Mawathe jijini Nairobi anasema Dk Besigye anatarajiwa kusafiri na ndege ya saa 12 saa za Afrika Mashariki.