Waziri Robertson: England itajitoa Fifa

Waziri wa Michezo Hugh Robertson ametoa ushauri wa umewezekano wa England kujiondoa Fifa iwapo Shirikisho hilo la Soka Duniani halitajibu tuhuma za rushwa ndani ya shirikisho hilo.

Haki miliki ya picha bbc
Image caption Lord Triesman

Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Soka cha England Lord Triesman, alidai wajumbe wanne wa Fifa waliomba "rushwa" ili waiunge mkono England katika hekaheka zake za kuwania kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2018.

"Nia ipo ya kujaribu na kufanya kazi kwa ajili ya mabadiliko ndani ya Fifa," Robertson aliiambia BBC Radio 4.

"Iwapo Fifa itathibitisha haiwezi kufanya hivyo, basi nitasema njia zozote zinawezekana kutumika."

Triesman, mwenyekiti wa zamani wa kamati ya England ya kuwania nafasi ya kuandaa Kombe la Dunia kwa mwaka 2018, amewatuhumu wajumbe wanne wa kamati kuu ya Fifa kwa kwenda "kinyume na maadili" wakati wa mchakato wa kutafuta nchi itakayoandaa mashindano hayo.

Wakati wa mahojiano na kamati maalum ya Bunge, juu ya kushindwa kwa England kupata nafasi ya kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2018 siku ya Jumanne, Triesman aliwashutumu makamu wa rais wa Fifa Jack Warner, Nicolas Leoz wa Paraguay, Ricardo Teixeira wa Brazil na Worawi Makudi kutoka Thailand, kwa kuomba "rushwa" ili waipigie kura England.

Rais wa Fifa Sepp Blatter ameahidi kuchukua hatua za haraka iwapo ushahidi utaonesha kulikuwa na kupindisha taratibu kwa shirikisho hilo la soka duniani.

Lakini Waziri wa Michezo Robertson ameitaka Fifa kuanzisha utaratibu wa uwazi katika mchakato wanaoutumia kuchagua nchi zinazoandaa Kombe la Dunia na vile vile kufuata utaratibu wa uwazi wa mageuzi uliofuatwa na kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC), kufuatia kashfa iliyojitokeza mwaka 2002 wakati wa kampeni za michezo ya majira ya baridi ya Olimpiki ya Salt Lake City.

"Jambo la kwanza ni kwamba tuhuma zimepelekwa mbele ya Fifa na ihakikishwe yanaendana na mtazamo wa FA," alisema Robertson.

"Inatulazimu kuweka ushahidi juu ya tuhuma hizo na nina matumaini Fifa itafuata mfano wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, ambao walilazimika kufuata mchakato kama huo baada ya michezo ya Salt Lake City.

England ilipigwa mweleka katika raundi ya kwanza ikiwa imepata kura mbili tu, wakatu Urusi ikapewa nafasi ya kuandaa mashindano hayo, wakati Qatar itaandaa mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2022.