Fifa yataka ushahidi wa tuhuma za rushwa

Fifa imekiandikia chama cha soka cha England, kikidai ushahidi kamili kuhusiana na tuhuma za rushwa ndani ya Shirikisho hilo la soka duniani.

Image caption Kamati ya England ya Kombe la Dunia

Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Soka cha England Lord Triesman alidai wajumbe wanne wa Fifa wataka wapewe "rushwa" ili waipigie kura England ya kuandaa mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2018.

Fifa imesema kuna "wasiwasi mkubwa" kutokana na madai haya mapya.

Fifa pia imetaka ipatiwe ushahidi kutoka gazeti la Sunday Times baada ya kuandika madai ya rushwa katika mchakato wa upigaji wa kura kwa ajili ya kuchagua nchi itakayoandaa Kombe la Dunia mwaka 2022.

Taarifa iliyotolewa na Fifa imesema: "Katibu Mkuu wa Fifa Jerome Valcke pia ametuma barua kwa gazeti la The Sunday Times kuwaomba waipatie Fifa ushahidi wowote walionao kuhusiana na taarifa iliyotolewa na Mbunge John Whittingdale."

Mbunge huyo wa Maldon, Essex, ni mwenyekiti wa kamati teule ya Bunge ya utamaduni, vyombo vya habari na michezo, ambapo Triesman alitoa madai yake siku ya Jumanne wakati kamati hiyo ilipomhoji kwa nini England ilishindwa kupata nafasi ya kuandaa mashindano ya soka ya Kombe la Dunia yatakayofanyika mwaka 2018.

Rais wa Fifa Sepp Blatter, anayewania kuchaguliwa tena mwaka huu, amesema Shirikisho lake halina budi kuchukua hatua za haraka kujibu tuhuma hizi mpya kabla ya mkutano mkuu wa Fifa wiki tatu zijazo.

"