John Demjanjuk apatikana na hatia

Mahakama moja nchini Ujerumani imempata na hatia John Demjanjuk, katika kusaidia kuwaua zaidi ya Wayahudi 28,000 katika kambi ya ki-Nazi wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Alichangia katika mauaji ya Wayahudi 28,000

Amehukumiwa kufungwa jela miaka mitano, mwaka mmoja pungufu, kama walivyotaka walioongoza mashtaka, na huenda akaachiliwa ikiwa atakata rufaa.

Demjanjuk, mwenye umri wa miaka 91, na aliyezaliwa Ukraine, alikuwa ni mlinzi katika kambi ya Sobibor, wakati Poland ilipokuwa chini ya wanajeshi wa ki-Nazi mwaka 1943.

Demjanjuk alikanusha kwamba alikuwa mlinzi, na kuelezea hata yeye alikuwa mfungwa, na aliteseka pia akiwa katika kambi hiyo.

Mawakili wa Demjanjuk wamesema watakata rufaa.

"Mahakama inaamini kwamba mtu anayejitetea...alikuwa ni mlinzi Sobibor kuanzia tarehe 27 Machi 1943 hadi katikati ya Septemba 1943", alielezea Jaji Ralp Alt.

"Kama mlinzi, alichangia katika mauaji ya watu 28,000", alisema.

Takriban watu 250,000 waliangamia katika vyumba vya sumu ya gesi Sobibor.

Demjanjuk anashtakiwa kwa kusaidia katika mauaji hayo, hasa watu 28,060 alipokuwa akifanya kazi kama mlinzi.

Bado haijafahamika wazi ikiwa Demjanjuk, ambaye familia yake inasema ni mgonjwa sana, atapunguziwa hukumu ya jela kwa kuzuiliwa muda mrefu, tangu alipokamatwa na kusafirishwa kutoka Marekani, mwaka 2009.