Taliban wakiri kufanya shambulio Pakistan

Mabomu mawili katika chuo cha kijeshi kaskazini magharibi mwa Pakistan yameua watu 80, polisi wamesema.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mmoja wa majeruhi

Watu wasiopungua 120 wamejeruhiwa katika mashambulio hayo katika mji wa Shabqadar, katika wilaya ya Charsadda.

Baada ya awali kudhani kuwa mabomu hayo yalikuwa yametegwa, sasa polisi wamesema yalikuwa na mashambulio ya kujitoa mhanga.

Taliban wa Pakistan wamesema wamefanya mashambulio hayo kulipiza kisasi cha kuuawa kwa Osama Bin Laden mapemwa mwezi huu.

Shambulio la Ijumaa lilikuja saa kadha kabla ya wakuu wa kijeshi kufika mbele ya bunge kuelezea hatua walizochukua kuhusiana na kifo cha Bin Laden.

Katika mkutano wa faragha, mkuu wa upelelezi Luteni Jenerali Ahmed Shujaa Pasha anaripotiwa kuwambia wabunge kuwa aliwasilisha ombi lake la kujiuzulu baada ya majeshi ya marekani kumuua Bin Laden, lakini mkuu wa majeshi alikataa ombi lake.